March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‎Sekiboko aishauri Serikali kuboresha kozi za VETA kwa maendeleo ya jamii




‎Sekiboko:Vyuo vya VETA vitumike kutatua changamoto za kijamii,kiuchumi

‎Na Joyce Kasiki, Chemba

‎KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imeishauri Serikali kuhakikisha vyuo vya ufundi stadi (VETA) vinatumika ipasavyo katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi zinazozikabili jamii kwa kuanzisha na kuimarisha kozi zinazoendana na mahitaji halisi ya maeneo husika.

‎ Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Husna Sekiboko,ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati katika Chuo cha VETA Chemba kilichopo wilaya ya Chemba mkoani Dodoma , yenye lengo la kujifunza na kujionea utekelezaji wa shughuli za Serikali katika vyuo vya ufundi stadi nchini.

‎Alisema kuanzishwa kwa kozi zinazozingatia changamoto, fursa na rasilimali zilizopo katika maeneo husika kutasaidia kuongeza mvuto kwa vijana wengi zaidi kujiunga na vyuo vya VETA, sambamba na kuchochea maendeleo ya jamii zinazovizunguka.

‎“Ni muhimu vyuo vya VETA vikaanzisha kozi zinazolenga mahitaji halisi ya wananchi wa maeneo husika ili vijana wapate ujuzi unaoweza kuwasaidia kujiajiri na kuchangia maendeleo ya jamii zao.”

‎Wakati huohuo, baadhi ya wabunge waliopata fursa ya kuchangia maoni yao, wameitaka Serikali kuhakikisha kupitia vyuo vya ufundi, inazalisha vijana wenye ujuzi wa vitendo unaowawezesha kuchangamkia fursa mbalimbali za ajira na ujasiriamali nchini.

‎Mmoja wa wabunge hao ni Mbunge wa Jimbo la Ukonga Bakari Shingo ambaue alosema vyuo vya ifundi vina nafasi kibwa ya kuzalisha wataalam wanaohitajika sokoni.

‎“Vyuo vya ufundi vina nafasi kubwa ya kuzalisha wataalamu wanaohitajika sokoni, hivyo tunahitaji kuona vijana wakitoka hapa wakiwa tayari kufanya kazi au kujiajiri.” alisema Shingo

‎Naye Mbunge wa Viti Maalum Asha Baraka alisema katika kutekeleza hilo,Serikali ihakikishe Makundi yote maalum yanapata nafasi ya kunufaika na makundi hayo.

‎“Serikali ihakikishe wanawake na makundi maalum wanapewa nafasi ya kunufaika na mafunzo ya ufundi ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.”alisema Baraka

‎Akijibu hoja za wabunge, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Khafidh Amir, alisema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kuboresha miundombinu, vifaa vya kujifunzia pamoja na mitaala ili vyuo vya VETA viendane na mahitaji ya soko la ajira.

‎“Serikali itaendelea kuwekeza katika vyuo vya VETA ili kuhakikisha vinazalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa ya soko la ajira.”alisisitiza Naibu Waziri huyo

‎Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Antony Kasore, alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali ili kuimarisha mafunzo ya ufundi stadi nchini.

‎“Tunaendelea kuboresha mitaala na miundombinu ili mafunzo yanayotolewa yawe na tija kwa mhitimu na Taifa kwa ujumla.”