March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rungwe yajikita kuboresha shule ya watoto wenye mahitaji maalumu

Na Esther Macha, TimesMajiraOnline,
Rungwe

HALMASHAURI ya Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya imepokea zaidi ya shilingi milioni 249 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya ukarabati na uboreshaji wa zahanati ya Shule Maalumu ya Watoto Wenye Ulemavu Katumba (2), iliyopo wilayani humo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za afya na mazingira ya kujifunzia kwa watoto wenye mahitaji maalumu.

Akizungumza na TimesMajira Online Januari 20, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Renatus Mchau, amesema kuwa ukarabati wa zahanati hiyo umefikia hatua za mwisho za umaliziaji.

Amesema kuwa Halmashauri hiyo ina Shule Maalumu ya Katumba (2) iliyopo katika Kata ya Ibigi, ambayo ina zaidi ya wanafunzi 250 wanaotoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya wilaya hiyo kwa ajili ya kupata elimu maalumu.

“Tunashukuru Serikali Kuu kwa kuendelea kutoa fedha za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kujisomea kwa watoto hawa wenye mahitaji maalumu,” amesema Mchau.

Ameeleza kuwa hivi karibuni Halmashauri imekamilisha ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua zaidi ya watoto 80, hatua ambayo imeongeza uwezo wa shule hiyo kutoa huduma bora. Aidha, Serikali Kuu imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala.

Kutokana na umuhimu na umaalumu wa shule hiyo, Mchau amesema Serikali Kuu ilitoa shilingi milioni 249 kwa ajili ya kuboresha zahanati iliyokuwapo awali, ambapo miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba ya mtumishi, jengo la wagonjwa na vyoo. Miradi hiyo ipo katika hatua za umaliziaji.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji huyo ametoa wito kwa wazazi na walezi wenye watoto wenye mahitaji maalumu kuwasiliana na Halmashauri ili waweze kusaidiwa kupata haki ya elimu na huduma muhimu, akieleza kuwa Serikali hutoa zaidi ya shilingi milioni 14 kila mwezi kwa ajili ya chakula na uboreshaji wa mazingira ya huduma katika shule hiyo.

Amesisitiza kuwa ni vyema wazazi kuwaleta watoto wao shuleni ili wapate elimu ya msingi itakayowasaidia katika maisha yao ya baadaye.

Mmoja wa wazazi kutoka Kata ya Ibigi, Zawadi Amanyisye, amesema uwepo wa shule hiyo umeongeza mwamko kwa baadhi ya wazazi kuwaleta watoto wao shuleni, ingawa bado kuna changamoto kwa wazazi wachache wanaowafungia watoto wao majumbani kwa hofu ya kubezwa na jamii.

“Mungu akishakupa mtoto huna sababu ya kumtenga au kumficha. Kuwafungia watoto ndani ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kupata elimu. Serikali inawekeza fedha nyingi kwenye shule hii, hivyo nawasihi wazazi tusiache kuwapeleka watoto wetu,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu ya Awali na Msingi wa Wilaya ya Rungwe, Kotasi Mbwilo, amesema Halmashauri inaendelea kuboresha miundombinu ya elimu kupitia Mradi wa BOOST, ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya na matundu ya vyoo katika shule mbalimbali wilayani humo.

Ameeleza kuwa katika Shule ya Mahitaji Maalumu Katumba (2), Serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 88 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu na matundu ya vyoo, ambapo miradi hiyo ipo katika hatua za ukamilishaji.