Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WAZIRI wa Madini,Anthony Mavunde ametoa maagizo mbalimbali ikiwemo kuwataka Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa nchini kumpa taarifa ya orodha ya Leseni kubwa za utafiti ambazo hazifanyiwi kazi ndani ya siku saba na kuahidi kuzifuta zitakazobainika.
Mavunde ametoa maagizo jijini hapa leo Januari 22,2026 wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha Menejimenti cha Tume ya Madini kilichowakutanisha Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, kilicholenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka, pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika Sekta ya Madini.

Hatua hiyo ya Waziri inanakuja kutokana baadhi watu kumiliki leseni za uchimbaji bila kuzifanyia kazi jambo ambalo linaisababishia serikali hasara.
“Mimi kwa kushirikiana na Naibu Waziri tutahakikisha tunafuatilia kila leseni. Zile zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitafutwa na maeneo hayo kupewa wachimbaji wadogo wa madini,” amesema.
Vilevile amemtaka Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha kuwa kabla ya Juni 30, 2026, mfumo wa e-leseni unaowezesha wateja kupata huduma bila kufika ofisini unaanza kufanya kazi kikamilifu, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kupunguza urasimu katika utoaji wa huduma.
Vilevile, Waziri Mavunde amewataka wamiliki wa leseni za madini kuhakikisha wanazifanyia kazi leseni walizopewa, akionya kuwa leseni zitakazobainika kutofanyiwa kazi zitachukuliwa hatua ikiwemo kufutwa na kupewa wawekezaji wengine wenye dhamira ya dhati.
Pia amewaagiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuwasilisha kabla ya Februari 28, 2026, taarifa ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya wanawake na vijana kupitia Mradi wa Mining for a Brighter Tomorrow (MBT).
“Ifikipo Februari 2026 nitaanza oparesheni maalumu ya kukagua leseni hizo na kuzifuta zitakazobainika kutofanya kazi”amesema.

Hata hivyo amewataka Maofisa hao wa Madini kuwachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya Maofisa wa chini ambao wamekuwa wakichafua Ofisi zao na kusababisha migogoro kutokana na kujimilikisha Leseni za uchimbaji kwenye maeneo ambayo tayari yana wachimbaji.
Mavunde, amesema Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa ambao ofisi zao zitabainika kuhusika au kusababisha migogoro katika shughuli za uchimbaji wa madini, akisisitiza ulazima wa kuzingatia kikamilifu Sheria na Kanuni za Madini katika utekelezaji wa majukumu yao.
Waziri Mavunde amesema kumekuwepo na baadhi ya maafisa katika Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa wanaochangia migogoro ya mara kwa mara kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini kwa kutoa leseni kwa waombaji wasiostahili, hali inayosababisha malalamiko na migongano baina ya wachimbaji.“Nikiona kwenye ofisi yako kuna migogoro ya wachimbaji wa madini na kujiridhisha bila shaka kuwa ofisi inahusika, sitasita kuchukua hatua kali ikiwemo kukuondoa kwenye nafasi uliyokuwa nayo,” amesisitiza.
Ameaguza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kuhakikisha wanazingatia misingi ya haki, uwazi na weledi katika utoaji wa huduma, sambamba na kuhamasisha wananchi wengi zaidi kuomba leseni za madini kwa kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya uwekezaji.
Katika kuimarisha utendaji kazi, Waziri Mavunde amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano miongoni mwa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, hususan katika kushughulikia changamoto za sekta, huku akiwahimiza kusimamia maadili ya watumishi walio chini yao, akibainisha kuwa wao ndiyo taswira ya Wizara ya Madini kwa wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amempongeza Waziri Mavunde kwa kuendelea kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa Wizara na taasisi zake zitaendelea kushirikiana kwa karibu ili Sekta ya Madini izidi kuimarika.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt. Janet Lekashingo, wameishukuru Serikali kwa maelekezo na maboresho yanayoendelea kufanywa katika utoaji wa huduma na upatikanaji wa vitendea kazi ndani ya Tume ya Madini.

“Katika kipindi cha nusu Mwaka wa Fedha 2025/2026,Tume imekusanya jumla ya Shilingi Bilioni663.94 sawa na ongezeko la asilimia 25.39,”amesema
Hata hivyo Katika kikao hicho Waziri Mavunde amekabidhi Magari 23 kwa Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa ambayo yatawasaidia katika kuboresha utendaji wa kazi zao.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi