

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, Patrick Kipangula, amefanya ziara ya kikazi katika baadhi ya vyombo vya habari mkoani Dodoma kwa lengo la kukagua utekelezaji wa sheria, kutoa maelekezo na kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kipangula alisema bodi imetoa tangazo rasmi linalowataka wote wanaofanya kazi za kihabari kuhakikisha wanakidhi vigezo vya kisheria, akisisitiza kuwa kufanya kazi za uandishi bila ithibati ya bodi ni kosa kisheria.
Alisema katika ziara hiyo wamebaini changamoto mbalimbali zinazovikabili vyombo vya habari, zikiwemo baadhi ya wafanyakazi kuwa na usajili uliosuasua au kutokukamilisha vigezo vinavyotakiwa. Kufuatia hilo, bodi imevipa vyombo hivyo maelekezo ya kitaalamu kuhusu namna ya kukamilisha taratibu za usajili na kuzingatia matakwa ya ithibati.
“Kazi ya bodi ni kuhakikisha taaluma ya habari inalindwa kama zilivyo taaluma nyingine, pamoja na kulinda maslahi ya wanahabari. Mtu yeyote anayetamani kufanya kazi za kihabari anatakiwa awe amethibitishwa na bodi,” alisema Kipangula.
Aliongeza kuwa bodi itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha maelekezo hayo yanatekelezwa ipasavyo, huku akiwataka wahariri kuhakikisha waandishi na wafanyakazi wote wanaojihusisha na kazi za kihabari katika vyombo vyao wana vitambulisho halali vya ithibati.
Kipangula alihitimisha ziara yake kwa kuweka mikakati ya kukuza na kuimarisha masuala ya kihabari nchini, ikiwemo kuongeza uelewa wa sheria na maadili ya uandishi wa habari.
Ziara hiyo ilifikia tamati katika ofisi za Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Nchini (UTPC), ambapo alikutana na Mkurugenzi wa Umoja huo Kenneth Simbaya na Maafisa wengine kwa mazungumzo kuhusiana na masuala ya kihabari.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina