Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imesema itaendelea kushirikiana na Nchi ya Marekani katika masuala mbalimbali ya maendeleo ambapo Marekani kupitia Wizara yake ya Madini na Nishati imekuja na program maalum lengo likiwa ni kusaidia ajenda ya kimaendeleo katika sekta ya madini.

Ambapo hivi sasa inatarajia kuongeza eneo la utafiti wa kina wa Madini kupitia Shirika la Madini STAMICO na GST kuchimba Madini ya Kinywe.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Januari 21,2026 na Waziri wa Madini Anthony Mavunde ambapo amesema Tanzania na Marekani zimeandaa mpango wa kupanua utafiti wa kina wa Madini ya Kinywe hatua inayolenga kuongeza maarifa ya kitaalamu na kubaini fursa mpya za maendeleo katika sekta ya madini.
Mavunde amesema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhakikisha rasilimali za madini zinatambulika kikamilifu na kutumika kwa manufaa ya Taifa na wananchi.
Mavunde amesema maeneo ya awali yaliyofanyiwa utafiti yanaonesha uwepo wa Madini ya Kinywe katika mikoa ya Lindi na Mtwara, na kwamba Serikali itaendelea kupanua wigo wa utafiti ili kupata takwimu kamili za kijiolojia.
Ameeleza kuwa Watanzania wanaomiliki leseni za uchimbaji wa madini watapewa kipaumbele katika mpango huo, ambapo Serikali itashirikiana na wataalamu wa Marekani kufanya uchambuzi wa kina wa rasilimali hizo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, jitihada hizo zinatarajiwa kuongeza uzalishaji wa madini hayo kwa siku zijazo, huku makadirio yakionesha kuwa ifikapo mwaka 2050, kiwango kikubwa cha Madini ya Kinywe kitaweza kuzalishwa kila mwaka.

Katika hatua nyingine, Mavunde ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia Wizara yake ya Nishati na Madini kwa kuendeleza ushirikiano wa kitaalamu na Tanzania, ikiwemo kusaidia mafunzo ya wataalamu wa ndani.
“Kupitia ushirikiano huo, Watanzania watanufaika na mafunzo ya siku mbili ya kuchambua na kutafsiri takwimu za kijiolojia (Geo Data), yatakayosaidia kuongeza ujuzi katika sekta ya madini, ” Amesema Waziri Mavunde.
Kwa upande wake, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andy Lentz, amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa ushirikiano katika utafiti wa Madini ya kinywe utakuwa kwa muda mrefu.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi