Na Joyce Kasiki, Tanga
TANGA: Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imesisitiza kuwa elimu ya bima kwa wananchi ni msingi muhimu wa kulinda maisha, mali na ustawi wa uchumi wa taifa, huku ikitoa onyo kali kwa makampuni ya bima yatakayokiuka sheria na miongozo ya utoaji wa huduma.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea mkoani Tanga kuanzia Januari 19 hadi 26, 2026, Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya, amesema bima si suala la hiari bali ni nyenzo muhimu ya kupunguza athari za majanga na hatari mbalimbali zinazowakabili wananchi na taifa kwa ujumla.
Dkt. Lupilya alitoa kauli hiyo mara baada ya Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mhe. Dadi Kolimba, kutembelea banda la TIRA katika maonesho hayo, akibainisha kuwa sekta ya bima ina mchango mkubwa katika kulinda shughuli za kilimo, biashara na uwekezaji.
Amesema TIRA haitavumilia makampuni ya bima yanayokiuka sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayehujumu maendeleo ya sekta hiyo.
“Makampuni yanayokiuka sheria yanarudisha nyuma maendeleo ya sekta ya bima na uchumi wa nchi kwa ujumla, hivyo hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria,” amesema Dkt. Lupilya.
Ameeleza kuwa kukosekana kwa uelewa wa masuala ya bima kunalazimisha serikali kubeba mzigo mkubwa wa kifedha wakati wa majanga, hali inayochangia kuongezeka kwa umaskini na kudorora kwa shughuli za kiuchumi.
Kwa mujibu wa Dkt. Lupilya, TIRA kwa kushirikiana na wadau wa bima itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuwajengea uelewa juu ya umuhimu wa bima kama nguzo ya ustawi wa taifa na chachu ya kukuza pato la taifa.
Aidha, amezitaka kampuni za bima kubuni bidhaa bunifu zinazokidhi mahitaji halisi ya wananchi, akisisitiza kuwa bidhaa za bima zinapaswa kumlenga mwananchi wa kawaida badala ya kulinda maslahi ya makampuni pekee.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi