Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline
SAYU Seni (91) mkazi wa Wilaya ya Bahi kijiji cha Makanda-Mvumi amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya makazi, kuingilia kati mgogoro wa shamba lake ambalo alinyang’anywa kinyume na Nzije Shanga pamoja na kumtendea kitendo cha ukatili yeye na familia yake.
Sayu anaeleza kuwa kitendo cha shamba lake na mali zake zote kunyang’anywa na Nzije kwa madai kuwa yeye anapesa na hakuna mtu wa kumfanya jambololote na kutoa vitisho kwa familia kumempelekea kukimbiwa na familia yake na kubaki pekee bila kujua ataishije na ataishi wapi.
Sayu ameeleza kuwa kitendo cha kunyang’anywa mashamba na mtu ambaye anajiita tajiri ni kumsababishia umasikini na kumfanya ashindwe kuhudumia familia yake.
“Vitendo vya uonevu vinavyoendelea kufanywa na Nzije vinachangia kumuathiri,kiuchumi,kijamii na Kisaikolojia jambo ambalo limepelekea familia kunikimbia na kujikuta nikiwa ombaomba mitaani licha ya umri wangu kuwa mkubwa.
“Pamoja na kutumia juhudi kubwa kudai haki yangu lakini hazijaweza kuzaa matunda kutokana na mtesi wangu kujivunia pesa zake alizonazo huku akiwa ananitishia kwa madai kuwa atafanya jambo lolote nikiendelea kumfuatilia”Ameeleza Sayu.
“Mimi niliamia Bahi mwaka 2009 baada ya kununua shamba kwa Buda na Msalali ambao ni wamiliki wa asili eneo ambalo nimekuwa nikilitumia kwa Muda mrefu na mwaka 2017 katika msimu wa kilimo nilisafisha eneo kidogo kwa ajili ya kuongeza wigo wa shamba na kufikisha ya jumla ya hekali kumi kwa ajili ya kilimo.
Kwa kuwa utaratibu wa kusafisha eneo kwa ajili ya kilimo unahitaji kupata kibali chenye thamani ya shilingi 5000 lakini kwa kuwa sikufuata utaratibu niliambiwa natozwa faini shilingi 300,000 na sikuwa na hiyo hela nikaanza kutengenezewa figisu”ameeleza Seni.
Kwa upande wake Nzije Shanga alipotakiwa kujibu malalamiko ya kumpora eneo Sayu Semi amesema kuwa yeye ni mmiliki wa eneo na alipewa na uongozi wa wilaya kwa kushirikiana na kijiji.
Hata hivyo hakutaka kuendelea kutoa ufafanuzi zaidi wa jambo hilo kwa madai kuwa yeye anashughuli nyingi za kilimo na ufugaji.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Makanda-Mvumi,Msafiri Makacha alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa mgogoro huo alisema kuwa mgogoro huo umetawaliwa na udugu na sintofahamu ya kimaamuzi.
Hata hivyo alisema kuwa ataendelea kuona namna ya kufuatilia jambo hilo ili kila mmoja apate haki licha ya kutokuwa na ufahamu wakutosha kama mlalamikiwa na mlalamikaji walisha malizana.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi