Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online-Nkasi
Balozi wa kudhibiti na kupambana na uvuvi haramu ukanda wa maziwa makuu Pascal Mwakatenya,ametoa wito kwa Maofisa usafirishaji (bodaboda), kutengeneza mazingira ya kujiheshimu na kuheshimu kazi yao.
Mwakatenya ameyasema wakati akizungumza na waendesha odaboda wa stendi kuu Namanyere wilayani Nkasi kwenye sherehe za kuukaribisha mwaka mpya wa 2026,zilizoandaliwa na bodaboda hao kama sehemu ya mkakati wa kuanza kazi hiyo katika msimu wa mwaka huu.
Amesema kuwa bodaboda ni kazi kama ilivyo kazi nyingine hivyo ni jukumu lao kuhakikisha heshima ya kazi yao inajengwa na wao wenyewe na kufanya kazi hiyo kwa weredi,kujiepusha na matendo yoyote maovu ili waweze kuheshimika na jamii.
Pia amewasisitiza kuendelea kufuata sheria za usalama barabarani kwani ndiyo njia ya kuepuka misukosuko isiyokuwa ya lazima ya kukamatwa na hata kutozwa faini badala ya muda huo kuutumia kujijenga kimaisha na kuweza kutunza vyema familia zao.
Sanjari na hayo amewahimiza kwenda mbele zaidi na kuweza kuendesha magari pamoja na kujihusisha na shughuli nyingine za ujasiriamali badala ya kuitegemea kazi hiyo pekee.
Awali bodaboda hao katika risala yao,wamebainisha kuwa changamoto waliyonayo ni ya mikataba kandamizi kati yao na wamiliki wa pikipiki na kuomba uwepo wa mikopo rafiki ikiwa ni pamoja na kutokuwa na bima.
Hivyo waliiomba Serikali kuingilia kati juu ya mikataba hiyo kandamizi kwani wanajikuta muda mwingi wakiutumia kumtumikia mmliki wa pikipiki na wao kuendelea kuwa masikini licha ya kufanya kazi hiyo kwa nguvu zote.
Kufuatia maombi hayo Mwakatenya aliomba suala la mikopo alibebe na kulipeleka kwenye mamlaka husika za Serikali huku akitoa fedha kiasi milioni 1,ili zisaidie baadhi ya bodaboda hao kulipia bima zao huku akiwahidi kuwasaidia hadi wote wawe na bima.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi