Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
KUELEKEA Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya,kaya 54 za wananchi wanaoishi katika mazingira magumu katika Jimbo la Uyole zimepatiwa msaada wa chakula na fedha ili kuwawezesha kusherehekea sikukuu hizo kwa furaha na matumaini, sawa na wananchi wengine.
Msaada huo umetolewa na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Uyole,Dkt Tulia Ackson, Desemba 21, 2025, mara baada ya kukabidhi vyakula na fedha kwa wananchi wenye hali duni za kimaisha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt.Tulia alisema mpango huo unalenga kuzifikia kata zote 13 za Jimbo la Uyole na kaya 130 kwa ujumla, ili kuhakikisha hakuna mwananchi anayesahaulika katika kipindi cha sikukuu.

“Mpango wetu ni kuzifikia kata zote 13 za Jimbo la Uyole na kaya 130 kwa ujumla. Tunatamani kila mmoja amtazame jirani yake ili katika kipindi hiki cha sikukuu kila mmoja aweze kutabasamu. Sisi tunafanya haya ili kuendelea kuwapa tabasamu ndugu zetu hawa,” amesema Dkt Tulia.
Ameongeza kuwa kupitia Taasisi ya Tulia Trust, wamekuwa na utaratibu wa kila mwaka wa kuwafikia wananchi wasiojiweza kuelekea Sikukuu ya Krismasi, ili nao waweze kufurahia kusherehekea kama ilivyo kwa wananchi wengine.
“Kwa siku ya leo tumefanikiwa kuzifikia kata sita za Jimbo la Uyole, na kaya 54 zimepatiwa vyakula pamoja na fedha kwa ajili ya mboga. Pia tumekutana na mdau mmoja ambaye ni msanii, aliyepita kutoka kwenye shughuli zake na kuguswa kwa kusaidia wahitaji walioko Mtaa wa Nsalaga. Hili ni fundisho kwa wengine nao kuguswa na kuwasaidia wenzetu,” amesema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mwansekwa, Juma Mwakalobo, amesema Dkt Tulia ana uzoefu mkubwa wa uongozi, akibainisha kuwa awali aliwahi kuongoza Jimbo la Mbeya Mjini lenye kata 36, na aliweza kuzisimamia vyema.

“Sasa anaongoza Jimbo la Uyole lenye kata 13, ambazo ni rahisi zaidi katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo. Kwa kata yetu, wanufaika 12 wamepata msaada wa vyakula na fedha,” amesema.
Ameongeza kuwa vijana wa Tulia Trust wamekuwa wakitembelea kata hiyo mara kwa mara, na mwezi uliopita walihoji idadi ya wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kusaidiwa sare za shule na daftari, ambapo jumla ya watoto 200 walibainishwa kunufaika.
Naye Mratibu wa Tulia Trust Kata ya Mwansekwa, Athuman Kapuya, alisema walibaini wanufaika 12 katika kata hiyo, ambao wamepangwa kupatiwa msaada wa vyakula na fedha kuelekea Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Kata sita zilizofikiwa katika awamu hii ni Mwakibete, Mwansekwa, Tembela, Mwasanga na Ilomba.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi