Na Mwandishi wetu,Timesmajira
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Kanda ya Pemba, Chausiku Kuya, ameahirisha kesi ya madai iliyofunguliwa na waliokuwa wagombea wanane wa Uwakilishi kupitia chama cha ACT WAZALENDO Kisiwani Pemba hadi tarehe 23 Desemba 2025.
Uamuzi huo ulifikiwa baada ya mawakili wa upande wa wadai kuomba kupewa muda wa siku saba ili kupitia majibu ya maandishi yaliyowasilishwa na upande wa utetezi na kuandaa majibu ya kinzani kwa kina.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Chama hicho Wakili Omar Said Shaaban, ambaye pia ni kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai, amesema kuwa ombi la muda huo lililenga kuhakikisha wanajibu hoja za utetezi kwa usahihi na kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria.

“Ikifika wakati huo, kila kitu kitakuwa kimekamilika, na Naibu Msajili atayawasilisha mafaili yote kwa Jaji Mkuu kwa ajili ya kupanga majaji watakaosikiliza kesi hizi,” amesema Wakili Shaaban.
Ameongeza kuwa wamejiridhisha na hatua hiyo ya Mahakama na sasa wanajipanga kikamilifu kwa hatua zinazofuata za mashauri hayo.

Wakili Shaaban aliwataka waliokuwa wagombea waliowasilisha madai pamoja na wafuasi wa chama cha ACT WAZALENDO kuwa watulivu na wenye subira wakati kesi hizo zinaendelea Mahakamani.
“Sisi kama mawakili wenu tunawahakikishia kuwa kila kitu kitafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu zote za kisheria zitazingatiwa,” amesisitiza.
Kwa upande wa Serikali, jopo la mawakili wa Serikali likiongozwa na Mbarouk Suleiman Othman kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Majimbo yanayolalamikiwa katika kesi hizo ni Kiwani, Mkoani, Chakechake, Chonga, Wawi, Kojani, Konde na Micheweni.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi