March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kuondoa urasimu kwa matumizi ya teknolojia ngazi ya serikali za Mitaa

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imesema inaenda kuipata Tanzania wanayoitarajia ifikapo 2050 katika mapinduzi ya teknolojia na kuondoa urasimu katika utoaji huduma kwa wananchi hususani ngazi ya Serikali za Mitaa.

Hayo yalisemwa jijini hapa leo,Desemba 4 2025 na Mkurugenzi wa TEHAMA Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Erick Kitali mara baada ya Kongamano la 17 la wanazuoni wa Chuo cha Serikali za Mitaa(LGTI) Hombolo  linalokwenda na mada kuu ya Mapinduzi ya Teknolojia yatakavyotoa huduma kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa akimuwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Adolf Ndunguru.

Ili kuondoa urasimu kwa wananchi  Kitali amesema Rais alielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu namna gani ya kupeleka tabasamu kwa wanachi kwa kuondoa ucheleweshaji wa huduma na kuwapa huduma wananchi kwa wakati na kwa gharama ndogo na hayo yote yatafanywa na Waliofundishwa vizuri kwenye chuo cha Serikali za mitaa.

Aidha alisema kuwa wanajua namna gani watumishi hao waliofundishwa vizuri wanatumia teknolojia ya kisasa kuweza kutoa huduma ambazo wamezisema hapo na wataendelea kusisitiza hata kwa wale ambao wapo kwenye Ofisi tayari.

“Na kama mnavyofahamu wananchi wapo katika serikali za mitaa na pia kuna Kata,Vijiji,kuna Mitaa,kuna Vitongoji kwahiyo huduma zote wananchi wanazipatia kule kwahiyo kikubwa ambacho leo tulikuwa tunakiongelea namna ambavyo mapinduzi ya TEHEMA na yatasaidia wananchi kupitia wahitimu waliotoka katika Chuo hiki cha Serikali za Mitaa-Hombolo.

“Na ukiangalia wanafunzi wengi ambao wanatoka hapa Chuo chetu cha serikali za mtaa hapa Hombolo wanaenda kufanyakazi kwenye serikali za mitaa kwahiyo tunaona sasa namna wataenda kutumia kitu ambacho wamejifunza darasani,”alisema.

Vilevile Kitali alieleza kuwa Tanzania imefanya mapinduzi makubwa katika TEHAMA na kwenye eneo la utoaji huduma mfano afya ,utoaji huduma katika ukusanyaji wa mapato lakini utoaji huduma kama wa uuzaji viwanja ,upatikanaji wa leseni kidigitali ,upatikanaji wa viabali kama vya usafirishaji wanyama kidigitali ,huduma za kwenye elimu ambapo alisema kwasasa wanauwezo wa kujua watoto
ambao wameenda shuleni na ambao hawajaenda ili waweze kufuatiliwa.

Akizungumza kuhusiana na kongamano hilo Profesa Magreth Bushesha ambaye ni Naibu Mkuu wa Chuo Cha Serikali za Mitaa Hombolo,Taaluma,Tafiti na Ushauri amesema Mifumo ya TEHAMA imeboresha utoaji huduma  na kueleza uhaba wa Wataalam wa TEHAMA ambapo alisema kunachangamoto ya upatikanaji wa wataalamu katika mambo mengi ya teknolojia.

Hivyo Prof.Bushesha alisema wamechagiza serikali kuangalia namna ya kusomesha wataalamu maana teknolojia inakwenda mbio sana kwahiyo na wao lazima waende mbio katika suala zima la teknolojia.

Naye Mkufunzi toka Taasisi ya stadi za maendeleo Chuo Kikuu cha  Mzumbe,Profesa  Frank Theobard,ameishauri Serikali kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA ili kufikia uchumi wa kati. 

Alisema yeye kama akiwa muwasilishaji mkuu katika kongamano hilo amesema kuwa wasilisho lake lilikuwa linajaribu kuakisi kwa kiasi gani mapinduzi ya kitehama yaweza kuboresha ufikishwaji wa huduma kwa wananchi chini ya mamlaka za serikali za mtaa.

“Kama mnavyojua nchi yetu ilizindua dira ya maendeleo ya kuanzia 2025 hadi 2050 na lengo kuu ni kwajili ya kuboresha maisha ya wananchi kupitia jamii nakuangalia tulikotoka na tunakoenda tumepiga hatua suala zima la TEHAMA.Kwahiyo serikali imeweka msimamo mkubwa katika kuangalia namna tutakavyoweza kutumia mapinduzi ya TEHAMA kufikisha  kwa urahisi huduma kwa jamii,”alisema.