March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpogolo :Serikali za mitaa kutoka ilala shirikianeni na Tanesco kutoa huduma bora ya umeme

Na Penina Malundo,Timesmajira 

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka madiwani na wenyeviti wa serikali za mitaa kutoka Ilala, Temeke na Kigamboni kushirikiana kikamilifu na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ili kuwezesha utoaji wa huduma bora na ya uhakika ya umeme kwa wananchi.

Amesema kuwa sifa ya kiongozi bora ni kuishi na kutatua changamoto za wananchi, ikiwemo hitaji la umeme wa uhakika. Kwa msingi huo, amewataka madiwani na wenyeviti hao kuendelea kushirikiana na Tanesco ili kuhakikisha changamoto za upatikanaji wa umeme zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mpogolo ametoa wito huo leo, Novemba 20, 2025, jijini Dar es Salaam wakati akifungua kikao kazi kilichoandaliwa na Tanesco kwa ajili ya kuwakutanisha viongozi hao wa mitaa kutoka maeneo husika.

Mpogolo ameipongeza Tanesco kwa kuimarisha mahusiano na viongozi hao wa mitaa, hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali ya kuboresha huduma kwa umma.

Amesema viongozi hao wana jukumu muhimu katika kuhakikisha taarifa sahihi zinawasilishwa kwa mamlaka husika ili kuzuia vitendo vinavyohatarisha miundombinu ya umeme.

“Moja ya changamoto ni wananchi kuvunja nyumba au maghorofa bila kutoa taarifa Tanesco, au wamiliki wa maduka kujiunganishia umeme kiholela na kisha lawama kupelekwa kwa Tanesco. Ni wajibu wetu viongozi kulinda miundombinu ya serikali na kutoa taarifa kwa wakati ili kudhibiti vitendo hivi,” amesema.

Ameongeza kuwa kukutana na madiwani na wenyeviti wa mitaa ni hatua muhimu kwa kuwa wao ndio wanaojua kwa undani changamoto za wananchi, maeneo yanayojengwa, yanayobomolewa na mahitaji halisi ya umeme.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Tanesco, Irene Gowelle, amesema moja ya mikakati ya shirika hilo ni kukuza na kudumisha ushirikiano na wadau wake, wakiwemo viongozi wa mitaa ambao ni kiunganishi muhimu kati ya wananchi na serikali.

Amesema viongozi hao wanafahamu maisha ya wananchi wao na wana uwezo wa kueleza vyema matarajio na mahitaji ya jamii, hivyo ni muhimu kuimarisha mawasiliano kati yao na Tanesco.

Gowelle amebainisha kuwa kikao kazi hicho kimeandaliwa kwa lengo la kuendelea kujenga mahusiano mazuri na kutoa taarifa kuhusu maendeleo ya miradi mbalimbali ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa nchi nzima.

Amesisitiza kuwa huduma ya umeme katika jiji la Dar es Salaam inaendelea kuimarika na umeme upo wa kutosha na kwamba unatosha kuendesha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.