Na Jackline Martin, Timesmajira Online
Kamishna wa Bima nchini, Dkt. Baghayo Saqware, ametoa wito kwa wahariri na vyombo vya habari kufuatilia kwa karibu kesi za udanganyifu wa bima zinazoendelea katika mahakama mbalimbali nchini, ili kusaidia kuilinda sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Akizungumza jana katika mafunzo ya wahariri wa habari kuhusu masuala ya bima na umuhimu wa Taarifa ya Soko la Bima, Dkt. Saqware amesema ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) na vyombo vya habari ni muhimu katika kuhakikisha sekta hiyo inakuwa kichocheo cha maendeleo ya uchumi wa nchi.
“Vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kufichua wadanganyifu wa bima. TIRA ipo tayari kushirikiana nanyi katika kukuza uelewa na kutoa mafunzo mnapohitaji,” amesema.
Aidha, amewataka wahariri kuongeza weledi katika uandishi wa masuala ya bima na kutoa kipaumbele kwa habari zinazohusu sekta hiyo kwani zinagusa maisha ya wananchi wote kutoka kwa wafanyabiashara wadogo hadi wawekezaji wakubwa.

Dkt. Saqware pia amewahimiza wahariri kuendelea kutumia Taarifa ya Soko la Bima kama nyenzo muhimu ya uchambuzi wa habari, akisema taarifa hizo ni msingi wa uandishi wenye tija na unaozingatia takwimu sahihi.
Akizungumzia mwenendo wa sekta hiyo, Kamishna huyo amesema bima nchini imekuwa ikionyesha ukuaji mzuri mwaka hadi mwaka sambamba na mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia.

Kwa mujibu wa takwimu za karibuni, ongezeko la matumizi ya teknolojia, maboresho ya mifumo ya usajili na usimamizi wa kampuni za bima pamoja na kuimarisha udhibiti kumeongeza uaminifu na ushindani katika soko.
Kwa sasa Tanzania ina zaidi ya kampuni 40 za bima pamoja na mawakala, madalali na watoa huduma wengine wanaotoa bidhaa na huduma mbalimbali kwa wananchi. Hata hivyo, aliweka wazi kuwa bado kuna changamoto ya uelewa mdogo wa wananchi kuhusu umuhimu wa bima, eneo ambalo vyombo vya habari vinaweza kubadilisha kwa kutoa elimu sahihi.

Dkt. Saqware amesema sekta ya bima ina mchango mkubwa katika uchumi, kwani huduma za bima huwezesha uwekezaji, kuimarisha ujasiriamali na kutoa ulinzi kwa wananchi dhidi ya majanga kama moto, ajali, majanga ya asili na magonjwa.
Pia, katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama nishati, reli, barabara na viwanda, bima imeendelea kuwa nguzo muhimu ya kuhakikisha uwekezaji unafanyika bila kuhatarisha maisha ya watu na mali za taifa.
Ameongeza kuwa matumizi ya bima ya kilimo yameendelea kuwasaidia wakulima kupunguza hasara zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, hali inayochangia katika uhakika wa chakula nchini.

Aidha, ameainisha baadhi ya hatua ambazo TIRA imeendelea kuchukua ili kuifanya sekta ya bima kuwa imara, ya kisasa na yenye manufaa kwa wananchi. Hatua hizo ni pamoja na Kuboresha mifumo ya usimamizi na udhibiti kupitia teknolojia, Kuanzisha na kusimamia mifumo ya kidijitali ya usajili wa bima kama Online Registration System (ORS), Kuimarisha ukaguzi wa kampuni za bima ili kuhakikisha zinatimiza wajibu wao kwa wananchi, Kutoa elimu kwa umma kupitia redio, televisheni, mitandao ya kijamii na mikutano ya wadau na Kushirikiana na taasisi za kimataifa kuboresha uwezo wa sekta ndogo ya bima nchini.
Kwa upande wake Margaret Mngumi – Msuluhishi wa Migogoro ya Bima kutoka Ofisi ya Msuluhishi wa Migogoro ya Bima Tanzania (TIO) amesema TIO imekuwa kiungo muhimu kati ya wananchi, kampuni za bima na Serikali, na imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utatuzi wa migogoro ya bima hapa nchini.
Aidha amesisitiza kwamba Vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika Kufikisha elimu sahihi kwa wananchi kuhusu hatua za kudai fidia, Kusaidia kupunguza malalamiko yasiyo na msingi kwa kutoa taarifa sahihi, Kuelimisha umma dhidi ya udanganyifu wa madai ya bima (insurance fraud), na Kuimarisha uwajibikaji wa kampuni za bima kupitia uandishi wa uwazi na wa haki.
TIO inatambua nguvu mlizo nazo, na tungependa leo tuanzishe ukurasa mpya wa ushirikiano, ili kuboresha zaidi mazingira ya utatuzi wa migogoro ya bima kwa maslahi ya Watanzania.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi