Na Martha Fatael, TimesMajiraOnline
MKUTANO wa 30 wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) umeibua upya mjadala mzito kuhusu uwazi, ufuatiliaji na matokeo ya matumizi ya fedha za tabianchi kwa miradi ya maeneo ya milimani nchini Tanzania.
Tanzania imetajwa kupokea takribani dola za marekani milioni 304 (sawa na Shilingi Bilioni 775.2) katika miaka ya karibuni kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na athari za tabianchi katika milima ya Kilimanjaro, Meru, Usambara na maeneo mengine yenye umuhimu mkubwa wa mazingira, maji na kilimo.
Hata hivyo, hali halisi ya vyanzo vya maji, misitu na uchumi wa jamii za milimani imezua maswali makubwa kuhusu ufanisi na uwajibikaji wa fedha hizo.
Milima ya Tanzania ndicho chanzo cha zaidi ya asilimia 60 ya mito mikubwa, maji vijijini na mashamba yanayolisha mamilioni ya watu. Pamoja na umuhimu huo, uharibifu wa misitu, mmomonyoko, ukame na kuyeyuka kwa barafu ya Kilimanjaro vinaendelea kwa kasi.
Hii imeibua swali la msingi: kama kweli zaidi ya Dola za Marekani milioni 300 zimetolewa, mbona vyanzo vya maji vinaendelea kukauka na hali ya mazingira kuzorota?
Wakazi wa maeneo ya milimani wamesema hawajawahi kuona miundombinu, mafunzo wala fidia inayolingana na kiwango cha fedha kinachotajwa. Kwao, miradi mingi imebakia kwenye karatasi na ripoti, ikikosa matokeo yanayoonekana.
Ufuatiliaji umeonekana kuwa dhaifu, kwani wakazi wa maeneo ya milimani kama Rombo, Siha, Mwanga, Lushoto na Meru wanadai hawajawahi kuona tathmini za mara kwa mara zinazolingana na fedha zinazotajwa.
Badala yake wamekuwa wakishuhudia kuona miradi iliyokwama au isiyokamilika, ikiwamo ya kuvuna maji ya mlima, urejeshaji wa misitu na kinga za mmomonyoko ambazo hazikuonyesha matokeo yanayoweza kupimika.
Changamoto za uwazi na mgawanyo wa fedha
Changamoto kuu iliyobainika ni ukosefu wa uwazi kuhusu mgawanyo wa fedha kutoka katika vyanzo vikubwa vya kimataifa kama Green Climate Fund (GCF), Global Environment Facility (GEF) na Adaptation Fund katika ngazi za vijiji, wilaya, taasisi za mazingira, mamlaka za maji na taasisi za uhifadhi.
Ripoti zilizopo hazioneshi wazi fedha zilivyofika na nini kimefanyika katika maeneo lengwa. Wakazi wa milimani ambao wanashuhudia moja kwa moja athari za mabadiliko ya tabianchi wameendelea kuwa wa mwisho kupokea fedha na taarifa za miradi.
Uchunguzi unaonesha kuwa miradi kama urejeshaji wa misitu, uvunaji wa maji ya milima na ujenzi wa kinga za mmomonyoko ama imekwama, imechelewa au haikuonyesha matokeo ya msingi.
Wananchi waliohojiwa wamesema miradi mingi ni ya majina tu na haitoi matokeo yaliyotarajiwa. Kilio kikubwa ni kwamba jamii zinazokabiliwa na athari hizo ndizo zinazohusishwa kidogo katika maamuzi, licha ya kuwa na uelewa mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi kuliko wataalamu wanaoletwa kutoka nje. Kwao, fedha zinazoahidiwa kimataifa haziwafikii na zinabaki katika warsha, makabrasha na maofisini.
Mtazamo wa wajumbe wa kimataifa
Mjumbe Maalum wa Ujerumani Kuhusu Diplomasia ya Hali ya Hewa, Jennifer Morgan amesisitiza kuwa kila dola ya tabianchi lazima ionekane katika matokeo halisi ardhini, sio kwenye mlolongo wa taratibu au ripoti. Ameonya kuwa Afrika inakabiliwa na athari kubwa kuliko fedha inazopokea, hivyo miradi ya milimani lazima itoke kwenye ripoti na kuingia kwenye utekelezaji.
Waziri wa Mazingira wa Rwanda, Dkt. Jeanne d’Arc Mujawamariya ameonya kwamba nchi za Afrika Mashariki zimegeuzwa “maktaba za ripoti” badala ya mashamba ya matokeo. Ameitaka COP30 kuanzisha mfumo wa fedha unaofika kwa haraka na moja kwa moja kwa miradi.
Kutoka Tanzania, Dkt. Fred Manyika amesema miaka mingi imepita bila jamii za Rombo, Mwanga, Korogwe na Meru kuona uwekezaji unaolingana na takwimu za fedha zinazotajwa kimataifa. Balozi John Simbachawene ameongeza kuwa barafu ya Kilimanjaro haitasubiri taratibu za kimataifa na kudai fedha zifikishwe haraka kwenye miradi ya milimani.
Mratibu wa Kitaifa wa Climate Action Network (CAN), Tanzania Faustine Ngila Mshomba alisisitiza umuhimu wa fedha za tabianchi kufika moja kwa moja kwenye miradi ya milimani badala ya kuishia kwenye warsha na maandiko na kuwa zaidi ya asilimia 60 ya fedha hizo zinapotea kwenye taratibu zisizo na tija.
“Hatuwezi kuendelea kusikia kuhusu mabilioni wakati milima yetu inaendelea kuumia. Fedha lazima zichagie ardhini si tu ukutani mwa mikutano. Jamii zinazozunguka Kilimanjaro, Meru na Usambara lazima zione fedha hizi kwenye mabomba ya maji, misitu iliyorejeshwa na mabonde yanayofanya kazi. fedha za adaptation hazipaswi kujenga maandiko, bali kujenga ustahimilivu,” amesema Mshomba.
Mkurugenzi Mtendaji Forum for Climate Change, Tanzania (ForumCC), Stella Aron Msoffe amebainisha haja ya kuanzishwa kwa dirisha la ufadhili linalofikia jamii za milimani moja kwa moja akisema ina uelewa zaidi wa athari za mabadiliko ya tabianchi kuliko wataalamu kutoka nje.
“Jamii za Siha, Mwanga, Rombo na Lushoto zinaelewa athari za mabadiliko ya tabianchi zaidi kuliko mshauri yeyote aliyeletwa kutoka nje lakini wao ndio wa mwisho kupokea fedha, hili lazima libadilishwe kwenye COP30,” amesema Msoffe.
“Kila dola inayotoka Bonn au Washington, senti arobaini tu ndizo zinazoifikia ardhini Afrika na hata pungufu zaidi zinawafikia wakazi wa milima. Hii si tu kutokua na ufanisi, ni ukosefu wa haki.”amesisitiza Msoffe
Katibu Mkuu wa Pan-African Climate Justice Alliance (PACJA) Dkt. Mithika Mwenda ametumia mifano ya Tanzania na Kenya kuonyesha changamoto za mfumo wa ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Afrika haiombi huruma, inaomba uwajibikaji, hakuna sababu ya kutoa fedha za tabianchi kupitia mfumo unaokula zaidi ya kinachotolewa milima inaanguka, mito inapungua, barafu zinatoweka lakini ripoti zinaendelea kuongezeka, tunahitaji matokeo, si slaidi za PowerPoint,” amesema Dkt. Mwenda,
“Fedha lazima zichagie ardhini, si tu ukutani mwa mikutano….ikiwa COP hii haiwezi kuhakikisha hilo, basi COP hii lazima iangalie tena lengo lake.”amesema Dkt Mwenda
Maazimio ya COP30: hatua zinazopendekezwa
COP30 imependekeza kuanzishwa kwa dirisha maalumu la fedha ili kupunguza gharama za utawala hadi chini ya asilimia 10 na kuwezesha fedha kufika moja kwa moja kwa mamlaka za ndani na vikundi vya jamii.
Pia kuanzishwa kwa mfumo wa miradi inayoongozwa na jamii ili kuipa nafasi ya kuamua, kutoa ridhaa au kupinga miradi na asilimia 30 ya fedha kuelekezwa moja kwa moja kwao.
Hatua nyingine inayopendekezwa ni kuwapo kwa Mtandao wa Kimataifa wa Ustahimilivu wa Milima wenye lengo la kupima kwa usahihi athari za tabianchi katika milima kama Kilimanjaro, Himalaya, Andes na Alps, na kuweka mfumo wa kuripoti kwa uwazi na viwango vinavyofanana.
Sheria, sera na uwajibikaji
Sheria za UNFCCC na Mkataba wa Paris zinahitaji uwazi, matokeo na uwajibikaji. Tanzania kupitia Sheria yake ya Usimamizi wa Mazingira na kanuni zinazohusiana nayo, inatakiwa kusimamia fedha na matokeo katika ngazi zote, serikali kuu, halmashauri, Mamlaka za maji na wadau wa kimataifa.
Milima ya Kaskazini na Mashariki ni uti wa mgongo wa maji, misitu, kilimo na utalii. Dola milioni 304 si tarakimu pekee, bali ni uwekezaji katika maisha, uchumi na vizazi vijavyo. Bila uwazi, barafu itaendelea kuyeyuka, mito kupungua, vijiji kupoteza uchumi na misitu kuharibika.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi