March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakulima wa Karafuu Zanzibar wanufaika na malipo ya Kidigitali

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAKULIMA wa karafuu Zanzibar, sasa wananufaika na mapinduzi ya malipo ya kidigitali yaliyoletwa na Mixx kwa kushirikiana na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).

Akizungumza kwenye hafla ya ‘Vuna na Mixx’ iliyolenga kutoa zawadi kwa wakulima wa zao la karafuu kisiwani Pemba, Mkuu wa Wilaya ya ChakeChake, Pemba, Mgeni Khatib Yahya amesema,

“Leo tunashuhudia matokeo ya jitihada za dhati za Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi. Mfumo huu wa malipo kidigitali kutoka Mixx si tu umerahisisha namna ya kufanya malipo, bali umeongeza uwazi, ufanisi, na usalama wa fedha za wakulima wetu wa karafuu.

“Niwapongeze sana Mixx na ZSTC kwa ubunifu huu ambao umeleta tija kubwa kwa wakulima na uchumi wa Zanzibar kwa ujumla,” amesema Mgeni.

Mgeni aliwataka wakulima wa Karafuu wajitahidi kutunza mashamba yao na kupanda miche mingi zaidi ili wazalishe karafuu kwa wingi kufikia lengo la mwaka huu ambalo ni tani elfu ishirini.

Pia, ametoa wito kwa wakulima kuacha kusafirisha karafuu kimagendo kwani kunadidimiza uchumi wa Zanzibar.

Kupitia hafla hiyo yenye kaulimbiu “Vuna na Mixx”, wakulima waliotumia huduma ya Mixx kupokea malipo ya mauzo ya karafuu walikabidhiwa zawadi mbalimbali ikiwemo gari moja aina ya Suzuki Carry, pikipiki nne aina ya Boxer, baiskeli 20, na simu janja 30 kama ishara ya kuthamini bidii na uaminifu wao katika kutumia mfumo wa kidigitali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Yas Zanzibar, Aziz Said Ali amesema tukio hilo ni sehemu ya juhudi za Mixx kurudisha hisani kwa wakulima na kuendeleza dhamira ya kujenga uchumi wa kidigitali unaomgusa kila mwananchi.

“Tunaposherehekea wakulima leo, tunatambua mchango wao katika kukuza uchumi wa Zanzibar. Kupitia Mixx, zaidi ya shilingi bilioni 40 za malipo ya wakulima zimelipwa tangu mwezi Julai mwaka huu, huku mawakala zaidi ya 11,000 wakipata ajira na kipato. Vilevile, Serikali imeweza kukusanya zaidi ya shilingi milioni 192 kama kodi,” amesema.

Ameongeza kuwa, “Huduma za Mixx zimeleta uwazi, usalama, na ufanisi katika ulipaji wa wakulima. Tunataka kila mkulima wa karafuu awe sehemu ya mapinduzi haya ya kidigitali -mapinduzi yanayobadilisha maisha na kuongeza kipato”.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZSTC, Soud Said Ali amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya ZSTC na Mixx umekuwa mfano wa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa dira ya serikali ya kukuza uchumi wa kidigitali.

“Kabla ya mfumo huu, changamoto za ucheleweshaji wa malipo na usalama wa fedha zilikuwa kubwa. Lakini sasa, kila mkulima anapokea malipo yake papo kwa hapo kupitia simu yake ya mkononi. Hii ni hatua kubwa ya mageuzi,” amesema Soud.

“Zaidi, kupitia ushirikiano huu, tumefanikiwa kuwaunganisha wakulima na huduma nyingine kama bima ya afya na huduma za kifedha. Lengo letu ni kuhakikisha mkulima wa karafuu anastawi kiuchumi na kijamii,” ameongeza.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, wawakilishi wa sekta binafsi, wakulima wa karafuu kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar na wadau wa maendeleo.

#