Na Martha Fatael,TimesMajiraOnline
TANZANIA inatumia nafasi yake katika Mkutano wa 30 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) unaoendelea mjini Belém, Brazil, kusisitiza umuhimu wa utekelezaji wa haraka wa Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu (FRLD), ikitaka usimamizi wa fedha za tabianchi uwe wa haki, uwazi na unaoleta matokeo halisi kwa wananchi.
Hoja kuu ya ujumbe wa Tanzania ni kwamba, ingawa dunia inajadiliana kuhusu takwimu na ahadi, athari za mabadiliko ya tabianchi tayari ni uhalisia unaoharibu maisha ya watanzania, hasa kupitia ukame, mafuriko, na kuyeyuka kwa barafu za Mlima Kilimanjaro.

Ujumbe wa Afrika wahimiza uwiano
Mjumbe maalum wa Rais na mshauri kuhusu Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi, Dkt. Richard Muyungi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Majadiliano cha Afrika (AGN), amesema mafanikio ya FRLD yatategemea uwazi na kasi katika utoaji wa fedha.
“Kwa Afrika, mabadiliko ya tabianchi si dhana ya kesho. Ni janga la leo. Tunahitaji rasilimali zenye uhakika na si ahadi zinazopotea kwenye karatasi,” amesema.
Amesema Afrika inakabiliwa na majanga yanayorudiwa, ikiwamo mafuriko, ukame na vimbunga ambayo yanaharibu kipato, makazi na mifumo ya ikolojia, hivyo ni lazima mfumo wa fedha za tabianchi uakisi hali ya uhitaji wa dharura wa bara hilo.

Ufadhili wa haki na endelevu
Tanzania inataka bodi ya FRLD kuhakikisha upatikanaji wa fedha unakuwa wa wazi, unaotabirika na endelevu badala ya hali ya miaka iliyopita.
“Fedha lazima ziwe zenye uthabiti na zipatikane kwa wakati… mfumo huu hauwezi kuwa wa majaribio… ni suala la maisha ya watu,” amesema Dkt. Muyungi
Ameeleza kuwa mataifa ya Afrika yanataka kuona uratibu wa karibu kati ya FRLD, Mtandao wa Santiago, ambao unaratibu msaada wa kiufundi kwa nchi zinazoathiriwa na hasara na uharibifu wa tabianchi, na Mfumo wa Kimataifa wa Warsaw, unaotoa mwongozo wa kisera na kitaalam kuhusu namna dunia inavyokabiliana na athari hizo. Amesema vyombo hivi viwili vikitumika kwa uwiano vitasaidia kuondoa marudio ya majukumu ya taasisi na kupunguza ucheleweshaji wa misaada unaikumba Afrika mara kwa mara.

Kuondoa vikwazo vya utoaji fedha
Mwenyekiti huyo wa AGN amesema tatizo kubwa lililopo ni urasimu unaochelewesha upatikanaji wa fedha, ambapo nchi masikini mara nyingi hazina uwezo wa kitaasisi kushughulika na mifumo migumu ya kimataifa na kuwa tunahitaji njia rahisi na msaada wa kiufundi ili fedha hizi ziwafikie walio mstari wa mbele.
Sauti za kiraia zasisitiza uwajibikaji
Mkurugenzi wa Mtandao wa Kiraia wa Haki za Tabianchi (CAN Tanzania), Pendo Mwakisimba, amesema COP30 ni fursa ya kihistoria kwa dunia kugeuza ahadi za fedha kuwa vitendo.
“Kuna pengo kubwa kati ya maneno na fedha… Dunia inatoa ahadi za mabilioni, lakini kinachofika ni kidogo mno,” amesema.
Kwa mujibu wa CAN, wakati nchi zinazoendelea zinahitaji dola za marekani Bilioni 387 shilingi Trilioni 1,006.2 kila mwaka hadi mwaka 2030, fedha zilizotolewa mwaka 2022 zilikuwa Dola Bilioni 27.5 sawa na shilingi Trilioni 71.5 pekee, kiasi ambacho ni kidogo mno.
“Hilo ndilo linaloitwa pengo la haki za tabianchi… walioteseka zaidi wanapata kidogo zaidi,” amesema Mwakisimba.

Teknolojia na mikopo yenye masharti
CAN Tanzania inabainisha kuwa teknolojia rafiki kwa mazingira bado ni ghali na ngumu kupatikana, jambo linalozifanya jamii nyingi, hasa zilizo pembezoni, kushindwa kuhamia kwenye mifumo endelevu ya uzalishaji na matumizi ya nishati. Shirika hilo linasema kuwa bila uwekezaji wa kutosha, ruzuku na uhamishaji wa teknolojia kutoka kwa nchi zilizoendelea, juhudi za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi zitabaki kuwa nadharia.
“Teknolojia za umwagiliaji wa kisasa, nishati safi ya kupikia na mifumo ya tahadhari mapema ni muhimu, lakini gharama zake zinawazidi watu wetu. Tunahitaji teknolojia kwa masharti rafiki, si mikopo inayoongeza madeni,” amesema Mwakisimba
Wito kutoka kwenye uhalisia
Mkulima kutoka Mkoa wa Kilimanjaro, Neema Mushi amesema wanapokea taarifa za mabilioni ya fedha za tabianchi, lakini hawazioni mashambani na kuwa changamoto kubwa ni kutokuwepo kwa mifumo inayowafikia moja kwa moja wakulima wadogo, ambao ndio wanaobeba mzigo wa athari za mabadiliko ya tabianchi kama ukame na mabadiliko ya msimu wa mvua.
Neema ameongeza kuwa endapo fedha hizo zingeelekezwa ipasavyo, zingesaidia kuimarisha upatikanaji wa mbegu zinazostahimili ukame, miundombinu ya umwagiliaji na elimu ya kilimo hifadhi, hatua ambazo zingewaongezea tija na kupunguza hasara.
Mfanyabiashara wa mbao kutoka Mwanga, Abdallah Msangi amesema upungufu wa maji unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi umeathiri si tu kilimo, bali pia biashara na upatikanaji wa bidhaa muhimu na kuwa kupungua kwa maji kumepandisha gharama za uzalishaji, na hatimaye gharama za maisha kwa wananchi wa kawaida, ikiwamo kupanda kwa bei za chakula.
Kwa mtazamo wake, kama ilivyo kwa wakulima kama Neema, wananchi wa vijijini hawapati manufaa ya fedha za tabianchi wanazosikia kutajwa kwenye majukwaa ya kimataifa akisisitiza kuwa iwapo hazitaelekezwa moja kwa moja kwenye miradi inayogusa maisha ya watu, basi zitabaki kuwa takwimu tu zisizoleta mabadiliko kwenye jamii.

Uhusiano na sheria na mikataba ya kimataifa
Kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) na Mkataba wa Paris wa mwaka 2015, nchi zilizoendelea zina wajibu wa kutoa msaada wa kifedha na kiteknolojia kwa nchi zinazoendelea ili kuhimili athari za tabianchi.
Pia, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Tanzania ya mwaka 2004 na Kanuni za Usimamizi wa Taka za mwaka 2009 zinataka serikali kuhakikisha utekelezaji wa hatua za kukabiliana na uharibifu wa mazingira kwa ushirikiano wa kimataifa.
Wataalamu wa mazingira wanasema utekelezaji wa sheria hizi kwa uhusiano na mikataba ya kimataifa ndiyo utakaolifanya taifa lionekane kama mtekelezaji halisi wa makubaliano, si mtazamaji wa mikutano.
Wito wa uharakishaji
Katibu Mtendaji wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Umoja wa Mataifa, Simon Stiell, amesema dunia inapaswa kusonga mbele kwa kasi zaidi katika kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuongeza uhimilivu wa jamii zinazokabiliwa na athari za tabianchi.
Amebainisha kuwa licha ya hatua zilizopigwa, ikiwamo kupungua kwa utoaji wa gesi chafu kwa wastani wa asilimia 12 kufikia mwaka 2035, jitihada hizo bado ni ndogo ukilinganisha na ukubwa wa changamoto zinazokabili dunia. Anasisitiza kuwa mataifa yanahitaji kuongeza kasi ya utekelezaji ili kupunguza madhara yanayoendelea kuonekana katika maeneo mengi duniani.
Kauli hiyo inaimarisha wito wa Tanzania kwamba fedha, teknolojia na msaada wa kitaasisi lazima vitokane na misingi ya haki na usawa, ili kujenga taifa linaloweza kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwa vitendo.


More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi