March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jacqueline Mzindakaya ampongeza Dkt.Nchemba kuwa Waziri Mkuu

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, Jacqueline Mzindakaya, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua Dkt. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, pamoja na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha azimio hilo kwa kura za kishindo.

Akizungumza baada ya uteuzi huo, Mzindakaya alisema anampongeza Rais kwa kufanya chaguo sahihi, kwani Dkt. Mwigulu ni kiongozi mwenye uzoefu, mchapa kazi na mwenye maono makubwa ya kimaendeleo.

“Uteuzi huu ni wa busara na wa matumaini makubwa kwa taifa letu. Tumemsikia viongozi wengi wakizungumza kuhusu Dkt. Mwigulu, wote wakimuelezea kama mtu mwenye rekodi nzuri katika chama na serikali. Amekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza dira ya maendeleo ya Taifa,” alisema Mzindakaya.

Aliongeza kuwa Dkt. Mwigulu ni miongoni mwa viongozi waliochangia kwa kiasi kikubwa katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030, ambayo imebeba vipaumbele muhimu vya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

“Kwa kuwa ameshiriki kuandaa dira na ilani ya maendeleo, nina imani kubwa kuwa ataendelea kuongoza nchi katika njia sahihi ya kimaendeleo,” alisisitiza Mzindakaya.

Mbunge huyo pia aligusia hotuba ya Waziri Mkuu mpya, akisema ameguswa zaidi na sehemu iliyozungumzia ajira kwa vijana.

“Nikiwa kijana, nimeguswa sana na dhamira yake ya kujali kipengele cha ajira kwa vijana wa Kitanzania. Hilo limenipa matumaini makubwa kwamba serikali itazidi kuweka mikakati ya kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi na kimaendeleo,” alisema.

Mzindakaya alimaliza kwa kusema kuwa anaamini Dkt. Mwigulu, kutokana na uzoefu wake na uelewa wa hali ya maisha ya Watanzania wa kipato cha chini, ataendelea kuibua sera na mikakati itakayonyanyua maisha yao.

“Najua anajua uchungu wa maisha ya chini, hivyo ninaamini ataenda kuinua maisha ya Watanzania walio wengi,” alisema.