March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kigahe aweka bayana malengo ya utekelezaji Mufindi Kaskazini

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini mkoani Iringa, Mheshimiwa Exaud Kigahe, ameahidi kuendelea kulitumikia jimbo lake kwa bidii na uadilifu katika kipindi chake cha pili cha ubunge, akisisitiza kuwa miaka mitano ijayo (2025–2030) itakuwa ya kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Kigahe, ambaye amerejea bungeni baada ya kuhudumia wananchi wa Mufindi Kaskazini tangu mwaka 2020 hadi 2025, amesema jukumu lake la awali baada ya kuapishwa rasmi Novemba 11, 2025, lilikuwa kushiriki katika uchaguzi wa Spika wa Bunge na kushuhudia kuapishwa kwa wabunge wengine.

Aidha, amesema hatua inayofuata ni kuthibitisha jina la Waziri Mkuu ajaye, ambaye ataongoza utekelezaji wa ajenda za maendeleo za Taifa.

“Kwa kuwa nimekuwa sehemu ya Baraza la Mawaziri, nina matumaini makubwa kumpata kiongozi atakayeendeleza ajenda ya maendeleo ya Taifa ya 2020 pamoja na kutekeleza Ilani ya CCM, ambayo ndiyo dira ya serikali tunayoiunda,” amesema Kigahe.

Ameongeza kuwa anatarajia Waziri Mkuu mpya atasimamia maendeleo endelevu kwa kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amesema ameonyesha mfano wa uongozi bora na mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita.

“Mheshimiwa Rais Samia ameleta mageuzi makubwa ambayo hayajawahi kufanyika katika nchi hii. Miradi mikubwa ya barabara, maji, afya na elimu imetekelezwa pia katika Jimbo la Mufindi Kaskazini, jambo ambalo limebadilisha kabisa maisha ya wananchi wetu,” amesema.

Kigahe amesema katika kipindi cha kwanza cha uongozi wake, miradi kadhaa ya kimkakati imefanikishwa, ikiwemo ujenzi wa barabara za lami vijijini, miradi ya maji, sekta ya afya na elimu, ambayo amesema imeweka historia mpya tangu kuanzishwa kwa jimbo hilo.

Ameishukuru jamii ya Mufindi Kaskazini kwa ushirikiano waliompa katika kipindi kilichopita na kuwataka waendelee kushirikiana naye katika kutekeleza mipango mipya ya maendeleo.

“Naomba wananchi waendelee kuwa nami bega kwa bega. Tumefanikisha mengi kwa pamoja, na sasa tunaenda kukamilisha miradi mikubwa tuliyoianza. Nina imani katika kipindi cha miaka mitano ijayo tutapata mafanikio makubwa zaidi,” amesema kwa matumaini.

Amesema kuwa anaamini kipindi cha pili cha Rais Samia Suluhu Hassan kitakuwa na tija kubwa zaidi kwa taifa, na kwamba Mufindi Kaskazini itaendelea kuwa mfano wa mafanikio ya utekelezaji wa sera za maendeleo nchini Tanzania.