March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Mbeya Mjini aahidi kuibadilisha Mbeya ,aomba utulivu ,amani

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

MBUNGE   wa Mbeya Mjini, Patrick Mwalunenge, ameahidi kuleta mabadiliko makubwa katika jiji hilo kwa kulifanya kuwa kitovu cha uchumi na fursa za ajira kwa vijana.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuapishwa,  Mwalunenge alitoa shukrani kwa wananchi wa Mbeya Mjini kwa imani waliyoonyesha kwake kupitia kura nyingi zilizompa ushindi, pamoja na chama chake cha Chama Cha Mapinduzi (CCM) chini ya Mwenyekiti wake Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumteua na kumpa dhamana ya kupeperusha bendera ya chama hicho.

 “Nawashukuru sana wananchi wa Mbeya Mjini kwa kuniamini. Shukrani pia kwa chama changu kwa kuniamini. Ahadi yangu ni kutekeleza yote niliyowaahidi  ikiwemo kutengeneza ajira kwa vijana na kulifanya jiji letu la Mbeya kuwa kitovu cha uchumi wa kanda ya nyanda za juu kusini,” amesema.

 Mwalunenge alisisitiza umuhimu wa umoja na ushirikiano kati ya wananchi na viongozi katika kufanikisha maendeleo ya jiji hilo.

 “Tunakwenda kuunganisha Mbeya Mjini iwe moja. Tufikirie pamoja na tushirikiane. Yale ambayo yapo ndani ya uwezo wangu kama mbunge nitayasukuma, na yanayoeezekana kufanyiwa na wananchi watafanya kwa nafasi yao Ili kuleta maendeleo kwa haraka.

Mbunge huyo pia amewataka vijana kulinda amani, akisema kuwa hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila amani.

 “Mambo yote tuliyopanga hayawezekani kama hakuna amani. Nawaomba vijana wa Mbeya walinde amani, kwani bila utulivu hakuna uchumi, hakuna ajira, hakuna mafanikio,” alisisitiza.

Aidha amesema  kuwa dira yake ya miaka mitano ni kuhakikisha wananchi wa Mbeya Mjini wananufaika kiuchumi.

“Mikakati yangu yote inahusu pesa ,nataka wananchi wapate pesa, waweze kuendesha maisha yao. Mbeya mpya ninayoiona ni yenye watu wanaojitegemea kiuchumi,” alisema kwa kujiamini.

Mbunge huyo alihitimisha kwa kueleza matumaini yake kuwa Bunge litakuwa chachu ya uwajibikaji na ushirikiano katika kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutekeleza majukumu yake ipasavyo.