March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DED Mbeya DC akabidhi vitendea kazi kitengo cha mawasiliano

Na Esther Macha,Timesmajira Online, Mbeya

MRUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Erica Yegella amekabidhi vitendea kazi vya kisasa kwa Kitengo cha Mawasiliano cha halmashauri hiyo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha mawasiliano na kuongeza ufanisi katika upashanaji wa taarifa kwa wananchi.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na Kamera aina ya 6D Mark II lenzi ya 24-105mm, stendi ya kamera, kadi ya kuhifadhia picha, speedlight, pamoja na kompyuta mpakato ya kisasa yenye uwezo mkubwa wa kuendesha programu za usanifu na uhariri wa picha na video (graphic designing).

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo,  Yegella amesema utoaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya mikakati ya halmashauri yake katika kuhakikisha Kitengo cha Mawasiliano kinawezeshwa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, hususan katika kusambaza taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa umma.

“Tumeona umuhimu wa kuimarisha Kitengo cha Mawasiliano kwani ndicho kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi. Kupitia vifaa hivi, tunategemea kuona taarifa za halmashauri zikitolewa kwa haraka, kwa ubora na kwa usahihi,” amesema “Yegella.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano,Fatina Msangi amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa hatua hiyo muhimu ya kulipatia kitengo chake vifaa vya kisasa vitakavyorahisisha utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Tunampongeza na kumshukuru sana Mkurugenzi Mtendaji kwa kutuamini na kutuunga mkono kwa vitendo. Vifaa hivi vitatupa nguvu mpya na ari ya kufanya kazi kwa bidii zaidi katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati” amesema,”Msangi.

Aidha,Msangi ameongeza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi katika utayarishaji wa machapisho, picha, video na taarifa mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Halmashauri hiyo inaendelea kujipambanua katika kuboresha mifumo ya mawasiliano na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa wakati, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa  Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.