Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma
MBUNGE wa Segerea kupitia Chama cha CHAUMA, Agnesta Lambart, ameahidi kuwatumikia wananchi wake kwa bidii katika kipindi cha miaka mitano ijayo, akisisitiza kuwa kipaumbele chake kitakuwa ni kuboresha miundombinu ya Barabara , maji safi na salama, afya, elimu na kuinua uchumi wa wananchi wa jimbo hilo.
Akizungumza Leo Novemba 11,2025 na waandishi wa habari mara baada ya kuapishwa kuanza shughuli rasmi za kibunge jijini Dodoma, Lambart alimshukuru Spika wa Bunge, Mheshimiwa Zungu, akisema ana imani kubwa na uongozi wake kutokana na uzoefu wake mkubwa wa kisiasa na kiutendaji.
“Nina imani tutashirikiana kwa karibu kuhakikisha masuala ya nchi yanaenda vizuri. Spika Zungu ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa, na ninaamini tutaweza kuvuka vizuri katika kutekeleza wajibu wetu wa kibunge,” alisema.
Lambart alieleza kuwa ushindi wake mkubwa wa kura 256,000 katika uchaguzi uliopita ni ishara ya imani ya wananchi wa Segerea kwa sera na maono ya chama chake cha CHAUMA.
“Uchaguzi wetu ulienda vizuri sana. Wananchi walionesha imani kubwa kwangu kwa sababu ya uadilifu na dhamira ya kweli ya kuwatumikia,huu ni ushahidi kwamba Segerea iko tayari kwa mabadiliko ya kweli,” aliongeza.
Mbunge huyo, ambaye awali alikuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia CHADEMA, alisema uzoefu alioupata akiwa katika kundi dogo la upinzani bungeni umemjenga, na anaamini hata katika mazingira ya upinzani wachache, hoja zenye tija zinaweza kuleta mabadiliko makubwa.
“Si lazima tuwe wengi ili mambo yafanyike kwa ubora,katika uchache wetu, tutafanya kazi kwa umoja na kupeleka hoja zenye tija kwa maendeleo ya Watanzania,” alisema kwa kujiamini.
Akizungumzia vipaumbele vyake kwa jimbo la Segerea,Lambart alisema changamoto ya miundombinu mibovu na ukosefu wa maji safi na salama itakuwa ni ajenda yake ya kwanza bungeni.
“Jimbo la Segerea limesahaulika kwa muda mrefu barabara hazipitiki na wananchi hawana maji safi na salama. Serikali ina sera ya kumtua mwanamke ndoo kichwani, lakini kwa Segerea akina mama bado wana changamoto ya upatikanaji wa maji,nitahakikisha sera hiyo inatekelezwa kwa vitendo,” alisema.
Aidha, aliahidi kuimarisha uchumi wa wananchi, hasa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kwa kuhakikisha wanapata mikopo ya asilimia 10 inayotokana na mapato ya halmashauri bila urasimu.
“Nitahakikisha fedha hizo zinafika kwa walengwa na zinawainua kiuchumi. Uchumi wa Segerea lazima usimame,” alisema.
Kuhusu sekta ya elimu, Lambart alilalamikia mzigo mkubwa wa michango ya shule unaowakabili wazazi licha ya sera ya elimu bure.
“Nitaweka nguvu kuhakikisha michango hiyo inapunguzwa au kuondolewa kabisa. Wananchi wangu wengi wana kipato cha chini, hawawezi kuendelea kubebeshwa gharama zisizo za lazima,” alisema.
Aidha. Lambart alisisitiza kuwa katika kipindi chake cha miaka mitano, atahakikisha wananchi wa Segerea wanapata maendeleo yanayoonekana.
“Kipaumbele changu ni kuhakikisha Segerea inabadilika na inakuwa na miundombinu bora, maji safi, huduma bora za afya, elimu yenye ubora, na uchumi unaowanufaisha wote,” alisisitiza.
Xxxxxx

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi