Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
BODI ya Wakurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni Tanzu ya Uwekezaji ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA INVESTMENT LTD – TIL), imezinduliwa rasmi leo Novemba 10, 2025 jijini Arusha.
TIL, imezinduliwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa TANAPA, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali George Marwa Waitara.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Wadhamini, Jenerali Waitara ameipongeza bodi hiyo na kuwataka kuimarisha uongozi wa kitaalamu katika kusimamia maendeleo ya kampuni hiyo.

“Bodi ya Wadhamini inawapongeza kwa kuchaguliwa kuongoza kampuni hii. Twendeni pamoja kusimamia kwa weledi na uwazi miradi yote ya kampuni.
“Tukaimarishe ushirikiano kati ya Kampuni, TANAPA na wadau kwa misingi ya uwajibikaji, ubunifu na uadilifu,” amesema Waitara.
Ameongeza kuwa, bodi hiyo inatarajiwa kuleta ubunifu katika uwekezaji wenye tija, kujenga taswira chanya ya kampuni katika sekta za umma na binafsi.
Lakini pia, kutekeleza miradi inayoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwemo falsafa ya uhifadhi endelevu na wenye manufaa kwa taifa na jamii.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, CPA Mussa Nasoro Kuji amesema shirika linaendelea kutambua mchango wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji na mageuzi ya kiuchumi, hususan katika sekta za uhifadhi na utalii.
Mtendaji Mkuu wa TIL, Mhandisi Dkt. Richard Matolo amesema kampuni imejipanga kuleta mapinduzi katika sekta ya ukandarasi kwa kutumia utaalamu wa hali ya juu na vifaa vya kisasa.

“TIL tunao wataalamu wenye elimu na uzoefu mkubwa katika kazi za ukandarasi, na kampuni inavyo vifaa vingi vya kisasa. Tunaahidi kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu,” amesema Dkt. Matolo.
TANAPA INVESTMENT LTD (TIL) ni kampuni tanzu ya TANAPA iliyoanzishwa kwa lengo la kutekeleza miradi mbalimbali ndani ya shirika kwa gharama nafuu, pamoja na miradi nje ya shirika kama kitega uchumi.


More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani