March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali imechukua hatua kulinda umoja kitaifa

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Dodoma

MAKAMU wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesisitiza kuwa Serikali ya Rais, Samia Suluhu Hassan, imechukua hatua madhubuti za kulinda umoja wa kitaifa na kuhakikisha wananchi wanaishi kwa utawala wa sheria.

Kauli hiyo alitoa akiwa mwakilishi wa Rais Samia katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), uliofanyika kwa njia ya mtandao kutoka mkoani Dodoma.

Dkt. Nchimbi alibainisha kuwa moja ya dhamira kuu ya Rais Samia ni kuhakikisha mazungumzo ya maridhiano yanatekelezwa ipasavyo, ili Taifa liendelee kuwa na amani, mshikamano, na liwe mfano wa utulivu barani Afrika na duniani.

Aidha, Makamu wa Rais alihakikisha kuwa Tanzania ipo salama na tulivu, na tayari kuendelea kupokea wageni kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwa manufaa ya pande zote.