March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Kitila atoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu

Na Penina Malundo,Timesmajira 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, ametoa wito kwa watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Akitoa wito huo leo  kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, katika Kongamano la Kitaifa la Amani lililofanyika jijini Dar es Salaam, likiwa na kaulimbiu “Kupiga kura ni haki yetu, kuilinda amani ni wajibu wetu.”

Amesema kuwa kupiga kura ni haki ya kikatiba huku kulinda amani ni wajibu wa kila Mtanzania hivyo ni vema Watanzania kutumia uchaguzi kama jukwaa la kuimarisha maendeleo na utulivu wa taifa. 

“Maendeleo ni mchakato endelevu. Tutumie uchaguzi huu kuwachagua viongozi watakaotupeleka mbele katika dira ya amani na maendeleo tunayoitamani,” amesema.

Prof. Mkumbo ameishukuru Kamati ya Amani ya Kitaifa kwa kuandaa makongamano hayo nchini kote, kwani yamerudisha imani kubwa miongoni mwa wananchi kwa taasisi za dini na viongozi wa serikali.

Prof. Mkumbo amesema uchaguzi ni fursa muhimu ya kutafakari historia na mustakabali wa taifa, akiwahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura. “Uchaguzi unahusisha tunu zetu za taifa: utu, haki, usawa, upendo, umoja, demokrasia, muungano na amani. Hizi ndizo nguzo zinazoitambulisha Tanzania,” amesema.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Mohamed Makusi, amesema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya amani na usalama. “Tutahakikisha kila mwenye haki ya kupiga kura anapiga kwa utulivu, na nchi yetu inabaki salama hata baada ya uchaguzi,” alisema Makusi.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano, Sheikh Alhad Mussa, amewaomba viongozi wa dini na wazazi kuendelea kuwaelimisha vijana kuhusu thamani ya amani. “Vijana wafahamu hawana nchi nyingine zaidi ya Tanzania. Kuiharibu amani ni rahisi, lakini kuirejesha ni vigumu. Tuwasihi wasikubali kupotoshwa,” amesema Sheikh Mussa.

 Rais wa Taasisi ya Amani,maridhiano na maendeleo Ya AFREDA Dkt.Denis Muchunguzi, amesisitiza kuwa taifa la Tanzania ni moja na linapaswa kulindwa kwa nguvu zote. “Tukiliacha likizama, tutazama sote. Amani ni takwa la maisha, katiba na dini zetu,” amesema.