Na Mwandishi Wetu,
MGOMBEA udiwani wa Kata ya Kiwalani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Iddi Burah, ameahidi kupambana kuhakikisha vijana wa kata hiyo wanapata fursa za ajira katika viwanda vilivyopo eneo hilo pindi atakapochaguliwa kuwa diwani katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam , Burah amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa Kiwalani ni ukosefu wa ajira licha ya kata hiyo kuzungukwa na viwanda vingi vinavyotoa nafasi mbalimbali za kazi.
Amesema hali hiyo imekuwa ikiwakatisha tamaa vijana wengi wanaoishi katika eneo hilo kwa kuwa ajira nyingi zinachukuliwa na watu kutoka nje ya kata hiyo.
“Kata ya Kiwalani tumezungukwa na viwanda vingi, lakini bado vijana wetu hawapati ajira. Wanaofanya kazi katika viwanda hivyo wengi wao wanatoka maeneo ya nje,” amesema Burah.
Burah alibainisha kuwa endapo atapewa ridhaa na wananchi kuwa diwani, moja ya kipaumbele chake kikuu kitakuwa ni kuimarisha mahusiano kati ya uongozi wa kata na wawekezaji ili kuhakikisha fursa za ajira zinatolewa kwa usawa, na vijana wa Kiwalani wanapewa kipaumbele.
“Nitahakikisha tunaunda mfumo rasmi wa ushirikiano kati ya kata na wamiliki wa viwanda, ili kila nafasi inayotokea vijana wetu wawe wa kwanza kunufaika,” amesema
Aidha, amesey viwanda vilivyopo Kiwalani vinahitaji aina mbalimbali za wafanyakazi wakiwemo madereva, mafundi, walinzi, wahudumu na watumishi wa kawaida, nafasi ambazo vijana wengi wa eneo hilo wangeweza kuzifanya bila hitaji la elimu ya juu.
“Viwanda hivi vina kazi nyingi ambazo hazihitaji shahada au elimu kubwa. Tatizo ni kukosekana kwa utaratibu mzuri wa kuwajumuisha vijana wetu kwenye mfumo wa ajira,” ameongeza
Burah amesema kuwa kukosekana kwa ajira kumekuwa chanzo cha kuongezeka kwa makundi ya vijana wasiokuwa na shughuli za kufanya, hali inayosababisha ongezeko la vitendo vya uhalifu, uvutaji wa dawa za kulevya na ujambazi wa barabarani maarufu kama panyaroad.
“Tukiwapa ajira vijana wetu watakuwa bize, watakuwa na kipato, na maisha yao yatabadilika. Hiyo ndiyo njia bora ya kupunguza uhalifu na kukuza uchumi wa kata yetu,” amesisitiza
Mbali na ajira, Burah alizungumzia pia sekta ya elimu, akieleza kuwa tayari kuna mpango wa kujenga shule mpya ya sekondari ya ghorofa katika kata hiyo, ambayo itakuwa suluhisho la msongamano wa wanafunzi katika shule zilizopo sasa.
Amesema Serikali imetenga Sh milioni 500 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, na kwamba ujenzi unatarajiwa kuanza mara baada ya taratibu za manunuzi kukamilika.
“Elimu ni nguzo ya maendeleo. Kupitia shule hii mpya, vijana wa Kiwalani watapata nafasi zaidi za kusoma karibu na makazi yao na katika mazingira bora,” amesema
Burah ameongeza kuwa dhamira yake kama mgombea wa CCM ni kuhakikisha anashirikiana na Serikali na wadau wa maendeleo katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa Kiwalani, ikiwemo miundombinu, afya, na huduma za kijamii.
Aidha amewataka wananchi wa kata hiyo kumpa ridhaa katika uchaguzi ujao ili aweze kutimiza malengo hayo kwa vitendo na kuwaletea maendeleo yanayoonekana.
“Naomba wananchi wanichague kwa imani kwamba sauti yao haitapotea. Niko tayari kufanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano ili Kiwalani iwe sehemu ya mfano katika ajira na maendeleo,” amesema Burah.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako