Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Benjamin Kuzaga, amewataka wananchi mkoani humo kupuuza taarifa za upotoshaji zinazoenezwa mitandaoni zinazohamasisha watu kutoshiriki kupiga kura, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.
Kamanda Kuzaga alitoa kauli hiyo Oktoba 25, 2025, wakati akiongoza mbio za pole zilizoandaliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, chini ya uratibu wa Mkurugenzi Mtendaji wake, Erica Yegella, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea ushindi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kikanda uliofanyika Oktoba 14, 2025, na kuhamasisha wananchi kushiriki kupiga kura.
“Wananchi, Oktoba 29, 2025, jitokezeni kwa wingi kupiga kura kwa amani. Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu. Iwapo kutajitokeza viashiria vya vurugu, toeni taarifa mapema ili tuimarishe ulinzi,” amesema Kamanda Kuzaga.

Ameongeza kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ikisambaza taarifa za uongo kuhusu uchaguzi, lakini akasisitiza kuwa wananchi wasiwe na hofu kwani ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya Mkoa wa Mbeya.
“Wapo wanaodai kuwa tarehe 29 Oktoba ni siku ya maandamano. Hiyo si kweli. Wajibu wetu kama polisi ni kulinda raia na mali zao. Ukimaliza kupiga kura, rudi nyumbani au endelea na shughuli zako kwa amani,” amefafanua.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella, amewapongeza wananchi na watumishi wa halmashauri hiyo kwa kufanikisha ushindi wa Mwenge wa Uhuru, akisema ushindi huo ni wa heshima kwa wilaya, mkoa na kanda kwa ujumla.
Yegella pia amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, akibainisha kuwa vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi jioni.
“Lengo la mbio hizi za pole ni kuwakumbusha wananchi wajibu wao wa kikatiba wa kushiriki kupiga kura. Huu ni wakati wa kuchagua viongozi mnaowataka kwa amani na utulivu,” amesema .
Katika hafla hiyo, Yegella amemkabidhi Kamanda Kuzaga tuzo maalum kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ikiwa ni ishara ya pongezi kwa ushirikiano mzuri kati ya jeshi la polisi na halmashauri hiyo.
Mmoja wa wananchi wa Mbalizi, Yusuph Juma, amesema mbio hizo zimewapa hamasa kubwa ya kushiriki katika uchaguzi.
“Awali tulichukulia kupiga kura kama jambo la kawaida, lakini kupitia mbio hizi tumeelewa umuhimu wake. Ni wajibu wa kikatiba na tunapaswa kushiriki kwa amani,” amesema.
Mbio hizo zilihusisha wananchi, watumishi wa umma na vilabu mbalimbali vya riadha, zikianzia Mlima Reli na kuhitimishwa Uwanja wa Mahubiri, zikiambatana na michezo ya mazoezi ya viungo, kukimbia na yai na kufukuza kuku.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi