Fresha Kinasa TimesMajira Online Mara.
MGOMBEA Ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Bunda Mjini Ester Bulaya, amewasihi Watanzania kutojaribu hata kidogo kuingia katika mtego mchafu wa kuhatarisha amani iliyopo nchini, ambayo iliasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na kuwafanya Watanzania waendelee kuishi kwa umoja, amani na mshikamano.
Bulaya ameyasema hayo Oktoba 25, 2025 wakati wa zoezi la kufunga kampeni za uchaguzi mkuu waJimbo la Bunda Mjini, zilizofanyika eneo la Stendi ya Zamani Mjini Bunda, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi, wanachama wa CCM, wananchi pamoja na aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA na kutimkia CCM, Ezekiel Wenje.
Amesema amani iliyopo nchini inapaswa kulindwa na kila Mtanzania kwani ndiyo msingi wa maendeleo, na kwamba ikitoweka hakuna sehemu nyingine ya kukimbilia. Aidha, amesema kuwa wanaoendesha kampeni za kutaka kuharibu amani wengi wao wapo nje ya nchi
“Niwaombe ndugu zangu, mjitokeze kwa wingi kumchagua Dkt. Samia Hassan, mnichague mimi niwe Mbunge wenu, na muwachague madiwani wa Chama Cha Mapinduzi. Tuilindeni amani yetu ambayo Mwalimu Nyerere alituachia, na viongozi wote wamekuwa wakiilinda,” amesema Bulaya.

Ameongeza kuwa “Amani ikitoweka hatuna pa kukimbilia. Unaweza kuwa na pesa lakini bila amani huna sehemu ya kuzipeleka. Tusifanye kosa tukaipoteza amani. Leo tunaweza kuwa na uhuru wa kuongea chochote kwa sababu tuna amani, na nchi yetu inaendeshwa kwa misingi ya kikatiba. Waliopitia adha ya vita hawataki kusikia vita.”
Bulaya ameendelea kwa kusema kuwa wananchi wakimchagua ataenda kuwasemea kikamilifu bungeni, kwani anao uwezo madhubuti wa kujenga hoja. Amesema pia kuwa yuko kwenye chama chenye serikali, hivyo changamoto za wananchi zitapatiwa suluhisho kwani Dkt. Samia ni kiongozi msikivu, mnyenyekevu na anayejali maisha ya Watanzania kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Kuna changamoto ya miundombinu, naahidi nitakwenda kuiomba serikali iiwezeshe TARURA kwa kuipa fedha ili tumalize changamoto hii. Naamini pia tutakwenda kukamilisha miradi ya umeme kwenye kata za pembezoni, pamoja na kuiomba serikali ifufue hapa Bunda jineri moja kwa ajili ya kuwezesha vijana kupata ajira, pamoja na kupambania soko la kisasa kuongeza mapato na kukuza uchumi,” amesema Bulaya.
Aliyewahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye kwa sasa ni kada wa CCM Ezekiel Wenje , amesema serikali ya CCM chini ya uongozi wa Dkt. Samia Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika miradi ya maendeleo nchini, hivyo Watanzania wanapaswa kuichagua kwa kishindo Oktoba 29, 2025, ili iendelee kuwatumikia.
Akimnadi mgombea huyo, Wenje amesema“Bulaya ni mtu makini, mchapakazi na amekuwa kiongozi anayejipambanua kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo. Niwaombe wananchi wa Bunda Mjini wamchague kwa kura nyingi ili akawatumikie kwa dhati, akishirikiana na Rais Dkt. Samia na madiwani wa CCM.”
Ameongeza kuwa, “Niwaombe wananchi wote wa Bunda Mjini, kamchagueni Bulaya kwa kura nyingi Oktoba 29. Mpigieni kura Dkt. Samia Suluhu Hassan na madiwani wote wa Chama cha Mapinduzi kusudi waendelee kuleta maendeleo ya kweli. Chini ya Dkt. Samia tumeshuhudia miradi mikubwa ikitekelezwa inayogusa maisha ya Watanzania kwa kipindi cha uongozi wake. Tumpeni ushindi afanye hivyo miaka mingine mitano,” amesema Wenje.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT) Mkoa wa Mara, Nancy Msafiri, amewataka wananchi wa Bunda Mjini na Mkoa wa Mara kwa ujumla kutambua kwamba Chama Cha Mapinduzi ndicho chama pekee cha kuwaletea Watanzania maendeleo.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako