Na Bakari Lulela,Timesmajira
VIONGOZI wa chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) wa mkoa wa Dar es salaam wapatao 180 wamepatiwa Mafunzo ya awali ya usalama na Afya Mahali pakazi Ili kuwawezesha kuzishauri menejimenti za taasisi zao kuboresha mazingira ya kazi na hivyo kupunguza ajali na Magonjwa yatokanayo na kazi.
Mafunzo hayo yaliwahusisha wenyeviti na makatibu wa matawi yote 90 ya TUGHE ya mkoa wa Dar es salaam, yamefanyika Katika kikao kazi cha siku mbili (Oktoba 21 na 22, 2025) , Kibaha Mkoani Pwani ambapo viongozi wapatao 180 wameshiriki.
Pamoja na masuala mengine,mada mbalimbali zinazolenga kujenga uelewa wa jumla kuhusu masuala ya Usalama na Afya Mahali pakazi zimewasilishwa na wataalamu wa OSHA. Mada hizo ni pamoja na Dhana ya Usalama na Afya Mahali pakazi, uwakilishi na kamati za afya na Usalama Mahali pakazi, mifumo ya usalama na Afya Mahali pakazi pamoja na misingi ya huduma ya kwanza Mahali pakazi.
Wawasilishaji wa mada kutoka OSHA. Simon Lwaho na Moteswa Meda wamesisitiza washiriki kuwahamasisha wafanyakazi wenzao katika sehemu za kazi kujifunza kanuni bora za Usalama na Afya kutegemeana na shughuli zao za kila siku ili kupata mbinu za kujilinda kujilinda dhidi ya vihatarishin mbalimbali vya Magonjwa na ajali Mahali pakazi.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha kikao kazi cha viongozi hao, Mtendaji Mkuu wa wakala wa Usalama na Afya Mahali pakazi (OSHA) Khadija Mwenda, aliyekuwa mgeni rasmi katika wa hafla ya kufunga kikao kazi hicho , amesema viongozi hayo wanayo nafasi muhimu katika kushawishi menejimenti za taasisi zao kuboresha ya kazi Ili kuleta ustawi wa wafanyakazi.

“Kupitia kikao kazi hiki tumewaeleza wenzetu wa TUGHE jitihada za serikali katika kuimarisha afya na Usalama na ustawi wa wafanyakazi ambapo mbali na kuiwezesha OSHA kusimamia uzingatiaji wa taratibu za Usalama na Afya, masuala haya yamejumuishwa katika kanuni za kudumu za utumishi wa umma.Aidha , uzingatiaji wa masuala ya Usalama na Afya unaangaliwa katika ukaguzi wa CAG pamoja na Tume ya utumishi wa umma,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA.
Aidha, kiongozi huyo mkuu wa OSHA nchini,Mwenda ameahidi kuendelea kushirikiana na TUGHE pamoja na vyama vingine vya wafanyakazi katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi nchini wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na kanuni bora za Usalama na Afya zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao ya msingi katika hali ya usalama na kubakia na Afya njema.

Mwenyekiti wa Tughe mkoa wa Dar es salaam, komredi Brendan Maro ameeleza OSHA kama mdau muhimu katika utekelezaji majukumu ya chama chao.
“Tunawashukuru sana OSHA kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakitupatia katika utekelezaji wa majukumu yetu hususani suala la kutoa elimu kwa wanachama wetu ambao ni wafanyakazi,” amesema Komredi Maro.

Akitoa neno la shukrani, mwakilishi wa washiriki wa Mafunzo hayo Norbertha Sanga ambaye ni Katibu wa Tughe tawi la Mamlaka ya Hali ya hewa (TMA) amesema Mafunzo ya usalama na Afya ni muhimu kwa wafanyakazi na waajiri Ili kuwa na uzalishaji wenye tija.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi