Fresha Kinasa ,TimesMajira Online ,Mara.
BALOZI wa Poland nchini Tanzania, Sergiusz Wolski, amekabidhi rasmi Mradi wa majengo mapya ya kisasa kwa Kituo cha ‘Nyumba Salama Kiabakari’ kilichopo Wilaya ya Butiama kinachotoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia vitendo vya ukatili wa kijinsia kutoka katika familia zao.
Ambapo Mradi huo umejengwa kwa gharama ya Shilingi Bilioni 1.5 kupitia ufadhili wa Polish Aid kwa kushirikiana na Kiabakari Foundation.
Kituo hicho kinamilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, ambalo linafanya kazi ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia Mkoani Mara. Mradi huo ulitekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili, unajumuisha miundombinu ya mabweni mawili ya kulala wasichana waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni, jengo la utawala, bwalo la chakula, karakana mbili, jengo la kupumzikia, uwanja wa mpira wa netiboli, uzio wa usalama na choo chenye matundu matano.

Akizungumza Oktoba 19, 2025 wakati wa hafla ya makabidhiano ya majengo hayo Kituoni hapo,Balozi Wolski amepongeza kazi kubwa inayofanywa na shirika hilo katika kusaidia kufanikisha ndoto za wasichana waliokumbwa na ukatili. Amesema Serikali ya Poland imekuwa ikijikita kusaidia miradi yenye kugusa jamii moja kwa moja, na iliamua kufadhili ujenzi wa majengo hayo ili kuwaweka salama wasichana wanaokimbia vitendo vya ukatili.
“Tatizo la ukatili wa kijinsia halipo tu Tanzania bali ni changamoto ya kimataifa. Nawapongeza pia Serikali na wadau mbalimbali wa Mkoa wa Mara kwa kushirikiana kikamilifu katika jitihada za kumaliza vitendo hivi,” amesema Balozi Wolski.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Thecla Mkuchika, amesema ujenzi wa majengo hayo umeongeza usalama kwa wasichana wakati wanapopatiwa hifadhi katika kituo hicho, na kwamba Serikali ya Tanzania itaendelea kuthamini juhudi za wadau wote wanaosaidia miradi ya kijamii.
Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly, amemshukuru Balozi huyo na Foundation Kiabakari kwa kusaidia kufanikisha mradi huo ambao una manufaa makubwa kwa wasichana. Ametoa wito kwa jamii kuachana kabisa na vitendo vya ukatili wa kijinsia, akieleza kuwa vinafifisha juhudi za serikali na kuzuia wasichana kufikia ndoto zao.

Ameongeza kwa kusema, “Naomba wadau wote wasimame pamoja kukemea vikali ukatili wa kijinsia mkoani Mara na nchini kote. Tunashukuru Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka sera ya elimu bila malipo, ambayo imefungua fursa kwa watoto wa kike kupata elimu.” amesema Rhobi.
Akisoma taarifa ya shirika hilo, Mkurugenzi Msaidizi, Domina Mabebe, amesema Hope for Girls and Women in Tanzania lilianzishwa mwaka 2007, likiwa na makao yake makuu katika Wilaya ya Serengeti, kwa lengo la kukabiliana na changamoto za ukatili wa kijinsia, hasa ukeketaji, ndoa za utotoni na manyanyaso dhidi ya wanawake na wasichana.
Amefafanua kuwa shirika hilo hutoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni, hufuatilia kesi mahakamani, hutoa msaada wa kisaikolojia na kisheria, na kufanya kampeni za uelimishaji kuhusu madhara ya ukatili. Pia hufanya uhamasishaji na kushirikiana na serikali za mitaa, viongozi wa dini na wazee wa mila kuleta mabadiliko ya kijamii.
Tangu kuanzishwa kwake, shirika limefanikiwa Kutoa hifadhi salama kwa zaidi ya wasichana 3,277 waliokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni, Kusaidia wasichana 1,232 kurejea shuleni na kuendelea na masomo, Kutoa mafunzo ya ujuzi kwa wasichana 3,262, Kupata majengo ya kisasa kupitia msaada wa Polish Aid, Kushirikiana na serikali katika kusimamia kesi za ukatili, Kufanikisha kampeni za uelimishaji kwa zaidi ya watu 100,000.

Hata hivyo, Mabebe ameeleza kuwa, shirika linakabiliwa na changamoto ya uhaba wa usafiri hasa wakati wa msimu wa ukeketaji, jambo linalokwamisha juhudi za kuwaokoa wasichana walioko hatarini. Huku akiongeza kuwa, kuanzia Novemba 2025, kutakuwa na ongezeko la watoto wanaohitaji hifadhi, jambo ambalo litaongeza gharama za uendeshaji wa kituo hicho.
“Hali hii inapelekea kuongezeka kwa mahitaji kama vile chakula, matibabu, vifaa vya kielimu, taulo za kike, na gharama za kuwaokoa wasichana walioko hatarini. Tunaomba wadau mbalimbali kushirikiana nasi kutatua changamoto hizi,” amesema Mabebe.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi