March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

VETA yawahamasisha vijana kuchangamkia fursa za ufundi Stadi

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online , Mbeya

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore, amewahamasisha vijana nchini kuchangamkia fursa za mafunzo ya ufundi stadi yanayotolewa na VETA, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kujiajiri.

Akizungumza alipotembelea banda la VETA katika Maadhimisho ya Wiki ya Vijana yaliyofanyika jijini Mbeya, CPA Kasore alisema ushiriki wa VETA kwenye maonyesho hayo unalenga kuonesha huduma zinazotolewa, mafanikio ya wanufaika wa mafunzo yao pamoja na kuhamasisha ushirikiano na wadau mbalimbali.

“Tumeleta bunifu na maonyesho mbalimbali yanayoonyesha namna tunavyotoa mafunzo kwa makundi yote, wakiwemo watu wenye mahitaji maalum, wanawake, na vijana kutoka mazingira magumu. Tunataka kila Mtanzania aone kuwa anaweza kupata ujuzi na kubadilisha maisha yake,” alisema CPA Kasore.

Alisema kupitia VETA, baadhi ya wanawake wamewezeshwa kuongeza ujuzi waliokuwa nao awali, hatua ambayo imewasaidia kuboresha shughuli zao za kiuchumi na kuongeza ubunifu katika bidhaa wanazozalisha.

Aidha, alieleza kuwa wakufunzi na wanafunzi waliopo katika vyuo vya VETA wamepata fursa ya kuonyesha umahiri wao kwa vitendo, kupitia kazi mbalimbali walizozibuni na kuzitengeneza kama sehemu ya mafunzo ya vitendo yanayotolewa na taasisi hiyo.

CPA Kasore alibainisha kuwa VETA pia imekuwa ikibuni suluhisho kwa changamoto za kijamii kupitia teknolojia rahisi na bunifu zinazotegemea mahitaji halisi ya jamii katika maeneo wanayohudumu.

Akizungumzia ushirikiano na wadau, alisema VETA inashirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo ofisi ya Waziri Mkuu na mashirika ya wanawake kama Samia Women Development Initiative, ambapo zaidi ya wanawake 15,000 wamepatiwa mafunzo ya ujuzi ili kuwasaidia kujikimu kimaisha.

“VETA bado inakaribisha wadau wengine kushirikiana nasi katika kufanikisha utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi, hasa kwa wananchi wenye mahitaji maalum na wale wanaotoka katika mazingira magumu,” aliongeza.

Alisema tofauti na vyuo vingine vya mafunzo, VETA ndiyo taasisi inayosimamia uandaaji wa mitaala ya ufundi nchini, hivyo kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanalingana na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadae.

CPA Kasore alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kugharamia mafunzo ya wanafunzi kwa kiwango kikubwa, huku VETA ikiwa na miundombinu ya kisasa inayojumuisha majengo bora na vifaa vya kufundishia vinavyowezesha utoaji wa mafunzo ya kiwango cha juu.

Amewahimiza wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalum kupeleka vijana wao VETA badala ya kuwafungia majumbani, akisema taasisi hiyo imejiandaa kuwahudumia na kuwa na miongozo kwa walimu katika kufundisha makundi hayo.