Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online , Mbeya
CHUO cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) mkoa wa Mbeya kimehitimisha mafunzo maalum ya ujuzi kwa wanawake kupitia mpango wa ‘Wanawake na Samia’ uliobuniwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Mafunzo hayo yaliyoanza rasmi 15 Julai 2025 yamehitimishwa mnamo 9 Septemba 2025 kwa mafanikio makubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika maadhimisho ya wiki ya vijana mkoani humo,Mkuu wa Chuo cha VETA Mbeya, Hassan Kalima, amesema kuwa mpango huo ulikuwa maalum kwa ajili ya kuwawezesha wanawake kupata ujuzi wa stadi mbalimbali za maisha na ajira, ikiwa ni juhudi za Rais Samia katika kuwawezesha wanawake kiuchumi.
“Mpango huu ulikuwa ni neema kwa wanawake wa Mkoa wa Mbeya. Tulitarajia kuandikisha takriban wanawake 200 hadi 300, lakini mwitikio ulikuwa mkubwa sana ambapo tulisajili jumla ya wanawake 1,184. “Amesema
Amesema mafunzo hayo yalihusisha kozi zaidi ya 40 zikiwemo utengenezaji wa batiki, sabuni, vitafunwa, mapishi, ushonaji nguo, ujenzi, ufundi magari, udereva, na kozi nyingine fupi zinazotolewa na VETA. ambapo katika idadi hiyo ya waliojiunga, wanawake 1,063 walihitimu mafunzo kwa mafanikio makubwa.
“Wanawake waliohitimu walionyesha furaha yao kwa kupata ujuzi ambao hawakuwa nao kabla. Baadhi yao walitoa zawadi kwa mgeni rasmi kwa kumshonea nguo ya kitenge kama ishara ya shukrani kwa kupewa fursa ya kujifunza.”amesisitiza
Katibu wa kundi la ‘Wanawake na Samia’ Mkoa wa Mbeya Hamida Mbogo ambaye ni mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, alieleza furaha yake kwa kushiriki mafunzo hayo na kumshukuru Rais Samia kwa kufanikisha mpango huo.
Amewahimiza wanawake wote nchini kutumia fursa ya vyuo vya VETA vilivyopo nchi nzima kujifunza na kujiendeleza.
“Wanawake wengi wa majumbani sasa wanapaswa kutoka na kwenda kujifunza,VETA wanatoa mafunzo mengi ya ujuzi yanayoweza kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja, Wanawake waliokuwa wakipika keki zisizo na ubora sasa wamejifunza na wanaweza kuboresha bidhaa zao,” amesema Hamida.
Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa VETA CPA Anthony Kasore, amesema kuwa lengo la awali la mpango huo lilikuwa kuwafikia wanawake 3,000, lakini kutokana na mwitikio mkubwa, sasa VETA inalenga kuwafikia wanawake 15,000 kote nchini.
“Sisi kama VETA tupo tayari kutoa mafunzo kulingana na mahitaji ya wananchi,Milango iko wazi. Wananchi waje watueleze aina ya mafunzo wanayohitaji, nasi tupo tayari kuwapatia,” amesisitiza Kasore.

More Stories
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani