Na Zena Mohamed,TimesMajira Online
BODI ya Usajili ya Wahandisi(ERB) imesema watu 5500 wanatarajiwa kushiriki katika Siku ya Wahandisi Nchini ambayo yatakuwa maadhimisho ya 18 tokea kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ambapo watu 2000 kati ya hao watashiriki kwa njia ya mtandao.
Pia wahandisi wataalam 630, wanatarajia kula kiapo cha utii wa taaluma yao ili kuhakikisha kuwa wanawajibika vyema katika taaluma zao,maamuzi pamoja na utendaji wao wa kihandisi wa kila siku.
Aidha, kiapo hicho kitatumiwa na vyombo mbalimbali kuwawajibisha pale watakapokiuka sheria na taratibu katika majukumu yao ya kila siku.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mkutano mkuu wa Bodi ya usajili Wahandisi nchini (ERB), Prof. Bakari Mwinyiwiwa amesema hayo jijini Dodoma wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wahandisi Tanzania mwaka 2021.
Prof.Mwinyiwiwa amesema, maadhimisho hayo yamepangwa kufanyika jijini Dodoma, kwa siku mbili kesho na keshokutwa katika ukumbi wa Jakaya Kiwete.
Amesema, pamoja na mambo mengine katika maadhimisho hayo jumla ya Wahandisi 630, watakula kiapo ya utii wa taaluma yao ili kuwafanya wawajibike katika utendaji wa mambo mbalimbali kwenye taaluma yao.
“Bodi ilianzisha utaratibu wa wahandisi wataalamu wote kula kiapo cha utii kwa taaluma yao na kwamba itakuwa ni mwiko kwao kukiuka miiko ya taaluma ya uhandisi,”amesema Prof. Mwinyiwiwa
Pia, alisema maudhui ya kiapo hicho yatakuwa ni Mhandisi kuanza kuitumikia taaluma kama mtaalamu, kiapo kitamkumbusha jukumu lake kitaalamu na umuhimu wa kuzingatia taaluma wakati wote.
Alifafanua kuwa kiapo kitaufanya umma ujenge imani kwa Wahandisi husika,kitatumika dhidi ya muhandisi atakapo vunja miiko na maadili ya taaluma katika kumchukulia hatua Mhandisi atake kiuka kiapo chake.
“Kiapo kitamlinda Mhandisi dhidi ya kulazimishwa kutenda mambo ambayo ni kinyume na taaluma yake,pia kitamkumbusha kuzingatia thamani ya fedha,usalama wa maisha ya binadamu na mazingira,kutoruhusu masuala ya jinai,kidini,jinsia,ukabila,rangi,milengoya kisiasa katika kutekeleza kazi zake za uhandisi,”alisisitiza Prof. Mwinyiwiwa.
Alisema katika majadiliano kitaaluma mada kuu itakuwa ni athari za mapinduzi ya nne ya viwanda kwenye miundombinu na viwanda kwa uendelevu wa uchumi wa kati.
“Pia zitakuwepo mada ndogo kamavile mafunzo na kujenga uwezo,miundombinu na maendeleo ya viwanda, namna na mbinu za kuhimili msongo wa mawazao kwa afya njema”alisema Prof. Mwinyiwiwa
Kadhalika alisema katika maadhimisho hayo kutakuwa na zoezi utoaji wa tuzo kwa Wahandisi na wahitimu wa taasisi.
“Hii ni moja ya shughuli kubwa itakayofanyika wakati wa kuadhimisha siku ya wahandisi kwa mwaka huu bodi itatoa tuzo kwa makundi ya wahandisi wahitimu kutoka vyuo vikuu na taasisi za uhandisi nchini mwaka 2019/20,”alisema.
Alieleza kuwa tuzo hiyo itakuwa ni kwa ajili ya Taasisi iliyotia fora kwenye maonyesho ya teknolojia na ubunifu,taasi iliyo tia fora kwenye maonyesho ya biashara,taasisi iliyotia fora kwenye maonyesho ya huduma za kitaaluma na taasisi iliyotia fora kwenye maonyesho ya uchuuzi.
Vilevile, alisema maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhuduriwa na watu zaidi ya 3,500 na wengine 2,000 watashiriki kwa njia ya mtandao kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Msajili Bodi ya usajili Wahandisi nchini Patrick Barozi, alisema kuwa hadi sasa wahandisi 17, wamechukuliwa hatua za kinidhamu kwa makosa mbalimbali.
Alisema moja katika makosa ambayo yameonekana kufanywa na wahandisi nchini ni kushindwa kusimamia kazi zao kwa viwango vilivyoelekezwa kwenye mikataba yao ya kazi.
More Stories
Wahakikishiwa usalama siku ya kupiga kura
CCM inabebwa na kazi nzuri za Rais Dkt. Samia-Makalla
Wananchi Babati wamshukuru Rais Samia kwa kuwafungulia barabara