January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Brela yaridhishwa na mwenendo wa usajili  majina ya biashara,makampuni Nane Nane Mbeya

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Mbeya

MKUU wa Kitengo cha Uhusiano Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Roida Andusamile amesema,zaidi ya wananchi 150 wakiwemo wafanyabiashara wamefungua makampuni na kusajili majina biashara zao katika maonyesho ya Wakulima Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari Andusamile amesema hadi kufikia Agosti 8,2023,wananchi wengi zaidi watakuwa wamesajili biashara zao .

MKUU wa Kitengo cha Uhusiano Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Roida Andusamile -kulia akizungumza na mteja aliyefika kwenye Banda la BRELA katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya

“Tangu amonyesho haya yalipoanza Agosti Mosi hadi leo Agost 7 mwaka huu,zaidi ya wananchi 150 tayari wamesajili majina ya biashara zao pamoja na kufungua makampuni,tunaamini mpaka kesho tutakapokuwa tunafunga maonyesho watu wengi zaidi watakuwa wamefika kwenye banda letu kusajili majina ya biashara zao na kusajili makampuni yao.”amesema na kuongeza kuwa

“Nahamasisha wananchi na wadau wengine waendelee kufika kwenye banda hili ili kupewa elimu lakini kusajili majina ya biashara zao BRELA,”amesema Roida Andusamile mkuu wa kitengo cha Uhusiano BRELA.

Mteja (mwenye flana nyekundu) aliyetembelea katika banda la BRELA katika maonyesho ya Wakulima Nane Nane katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya akisaini kitabu cha wageni

Amesema kuwa BRELA ni mdau mkubwa wa sekta ya kilimo nchini na kutumia fursa hiyo kuwataka wafike kwa wingi kwenye banda hili ili kupata huduma pamoja na mambo mengine yanayohusiana na masuala ya kilimo.

“Kama mnavyojua Serikali inalenga katika kuhakikisha wafanyabiashara hawapati mkwamo wowote kwa hiyo sisi tunawezesha biashara ,kuwezesha biashara ni pamoja na kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wanarasimisha biashara zao bila kupata mkwamo wala vikwazo.”amesema Roida na kuongeza kuwa

“Unaona hata hapa katika banda letu wadau mbalimbali wanapata huduma ambazo ni za usajili wa majina ya biashara,usajili wa kampuni ,na wakitimiza vile vigezo wanaondoka na vyeti wakiwa na furaha.”

Amesema kampuni hiyo haipo kibiashara bali ni taasisi ya kutoa huduma ndiyo maana gharama zao ni nafuu.