December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAC kukamilisha mradi wa Kimataifa Ziwa Victoria

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

Mkurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Kaimu Abdi Mkeyenge amesema moja ya mikakati ya Shirika hilo kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 kukamilisha Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria.

Mkurugenzi huyo ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya shgirika kwa mwaka wa 2023/24 huku akisema,mradi huo ni kukuza uwekezaji katika shughuli za usafiri wa kwenye maji na uvuvi.

Amesema,lengo la Mradi huo ni kushughulikia changamoto za usafiri wa kwenye maji , kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri majini na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria.

“Mradi huu unatekelezwa na nchi za Tanzania na Uganda na utagharimu  kiasi cha Shilingi bilioni 59.23 ambapo upande wa Tanzania gharama za Mradi ni Shilingi bilioni 19.97 zinazojumuisha gharama za kazi za ndani na sehemu ya mchango wa Tanzania katika kugharamia kazi za kikanda zinazofanywa kwa kushirikiana na Uganda.”amesema na kuongeza kuwa

“Mradi huu unatarajiwa kukamilika mnano mwezi Disemba, 2024 na tayari Mkandarasi ameshakabidhiwa maeneo ya kufanyia kazi katika mradi huu na Hadi sasa, Mkandarasi ameshaanza ujenzi kwa vituo vidogo vya Mara-Musoma, Kanyala na Nansio-Ukerewe”

Aidha Mkeyenge amesema,mpango mkakati wa utekelezaji katika mwaka wa fedha 2023/24  itasaidia uboreshaji na udhibiti wa huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji nchini sambamba na kuweka ushindani ili kuhakikisha huduma za usafiri majini zinakuwa endelevu.


Vile vile amesema mkakati mwingine ni kuratibu maandalizi ya Amri, kutoa maoni na kuwezesha uandaaji rasimu za Kanuni na nyenzo za utendaji zitoazo mwongozo kuhusu udhibiti huduma za usafiri majini, usalama na ulinzi kwa vyombo vya usafiri majini na uchafuzi baharini kutoka katika meli.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24 Shirika litasimamia utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa kuhusu Usafirishaji kwa njia ya Maji inayoratibiwa na Shirika la Bahari Duniani .

” Pia kushirikisha wadau katika kufanya mapitio na marekebisho ya Sheria na Kanuni mbalimbali, ikiwemo Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania, sura 415″. amesema 

Aidha ametumia nafasi hiyo kuishukuru sana Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha TASAC kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ikiwemo kusimamia Mradi wa Kimataifa wa Mawasiliano na Uchukuzi katika Ziwa Victoria.