January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Dom ahimiza matumizi ya pembejeo za ruzuku

Na Joyce Kasiki,Timesmajira Kongwa

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule  amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Kongwa na  Mkoa wa Dodoma kwa ujumla kutumia pembejeo za kilimo zitakazowawezesha kulima kwa tija.

Senyamule ameyasema hayo alipokuwa katika ziara yake ya kukagua shughuli za maendeleo wilayani humo.

Amesema,matumizi ya pembejeo za kilimo ndiyo yatakayowakwamua katika umasikini kwani watafanya kilimo chenye tija na watapata mazao ya kutosha.

Senyamule amesema,katika kuhakikisha hilo linafanikiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mbegu na mbolea ya ruzuku inayouzwa kwa bei nafuu Ili wakulima wote waweze kumudu na kununua pembejeo hizo.

“Sasa huu ni upendo ambao Rais wetu anauonyesha kwa wananchi wake,na sisi tunapaswa kumuunga mkono kwa kuzitumia  Ili tulime kidogo tuvune kingi.”amesistiza Senyamule

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Remidius Mwema amesema kumekuwa na changamoto kwa wakala aliyepangiwa kazi ya kusambaza mbegu wilayani humo na hivyo kushindwa kufanya kazi hiyo na kuleta usmbufu kwa wakulima.

“Kwa hiyo kwa sasa hatuna mtu anayesambaza pembejeo hizi ingawa tumeshazungumza na wakala anayesambaza katika wilaya ya Gairo ambaye ametuahidi kusambaza katika kata za Kongwa zinazopakana na Gairo.”amesema  Mwema

Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Mkoa  huo Benard Abraham amesema, suala hilo limeshamfikia mezani kwake huku akiahidi kulifuatilia suala hilo na kuhakikisha wakala anapatikana na ruzuku hiyo itapatikana katika eneo la Mbande suala ambalo Mkuu wa Mkoa Senyamule ametaka kupata taarifa ya upatikanaji wa ruzuku hiyo siku ya Junatatu ya Januari 9,2023.