January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

1&M Bank yazindua maboresho ya huduma za Rafiki Chat Bank

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

I&M Bank imezindua Maboresho ya Huduma za Kibenki kwa wateja wake kupita Rafiki Chat Bank, lengo ni kuchangia dira ya serikali ya Tanzania ya uchumi wa kidijitali chini ya ongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza na waandishi wa Habari jana wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa bidhaa za kidigitali wa I&M Bank, Adam Emmanuel alisema wao kama Benki wanahakikisha wateja wao wanapata huduma ambayo ni rafiki na ni rahisi kwa mahitaji yao ya kibenki.

Adam aliyataja maboresho ambayo wameyafanya katika Rafiki Chat Banking ikiwa ni pamoja na kuruhusu wateja wapya kufungua account popote alipo na kufanya usajili bila kufika Bank.

“Mteja anaweza kuingia kayika Whatsapp Banking yake akafungua account na akafanya usajili bila kufika Bank” Alisema

Katika kuhakikisha wateja wanapata huduma pale ambapo wanapata maswali au changamoto, Adam alisema kwa sasa wateja wataweza kuzungumza moja kwa moja na watoa huduma wao kupitia namba yao ya whatsapp Banking.

“Kama mteja atakuwa amepata changamoto atatuma kwenye namba yetu ya whatsapp banking ataweza kuwasiliana na mtoa huduma wetu na akapatiwa majibu ya moja kwa moja”

Kwa upande wa miamala, Adam alisema wameboresha kuhakikisha wateja wanaweza kufanya miamala mbalimbali ikiwemo miamala ya kwenda kwenye namba za simu lakini pia manunuzi ya muda wa maongezi, kulipia bili mbalimbali na hata kufanya miamala ya kibenki kutoka kwenye account yake moja kwenda account nyingine lakini pia kutoka kwenye account yake kwenda kwenye account za benki nyingine zilizopo nchini Tanzania.

“Tumehakikisha kwamba tunapunguza idadi ya hatua kwa kuhakikisha mteja anatumia muda mchache zaidi kukamilisha miamala, tutapata muda mzuri wa kuangalia hivyo basi anaweza kutumia muda mchache zaidi kumaliza muamala wake”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya I&M Tanzania, Zahid Mustafa alisema mbali na huduma hiyo pia wanajikita kwenye dhamira ya kuingia kwenye ulimwengu wa kidigitali ambapo wana huduma ya ‘KAMILISHA’ ambayo kwa mwezi Julai imewakopesha watanzania zaidi ya laki saba, mikopo zaidi ya Milioni 3 yenye zaidi ya shilingi Bilioni 13.

Naye Mkuu wa Kitengo cha wateja – I&M, zainab Maalim alisema takwimu zinazoonesha kwamba takribani asilima 33 ya watu Duniani wanatumia whatsapp kuwasiliana hivyo wao kama Benki wakaamua kuja na huduma hiyo ili kuwafikia watu hao.

“Mwaka huu tunatimiza miaka 50 hivyo tunasherehekea kwa kuwaletea huduma ambazo zinaangalia zaidi miaka 50 ijayo kwa kutambua kwamba watu wengi na Dunia inakoelekea ni
Kwenye kutumia mitandao hivyo huduma yetu hii inapenda kuwafikia watu hao kutokana na takwimu zinazoonesha kwamba takribani asilima 33 ya watu Duniani wanatumia whatsapp kuwasiliana hivyo na sisi tukaleta huduma hii ili kuwafikia watu hao”

“Tunawakaribisha wateja wetu pamoja na wateja ambao tungeweza kuwapata ili muweze kufurahia huduka hii na nyingine nyingi”

Mkuu wa kitengo cha wateja Rejareja na huduma za kidigitali, Simon Gachahi alisema kufanya kazi na serikali imewasaidia kwani wamekuwa wakiingia makubaliano nao ili kueneza miamala ya Benki

“Kupitia huduma hii ya whatsapp chat banking mwezi septemba tutafungua malipo ya kiserikali ambapo mteja ataweza kulipa kodi na
Malipo Mengine ya kiserikali kwa kutumia whatsapp Banking” Alisema