January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

18 wajeruhiwa kwa kuangukiwa ukuta kanisani

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Katavi

WATU 18 wakiwa ndani ya ibaada ya Jumapili katika kanisani la Free Pentekoste Church of Tanzania(FPCT)wamejeruhiwa na kulazwa katika kituo cha afya Inyonga Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, ACP Benjamin Kuzaga majeruhi hao wametokana na mvua kubwa kunyesha iliyoambatana na upepo mkali na kusababisha kuaguka kwa jengo la kanisa hilo lililopo katika kijiji cha Kamsisi Kata ya Kamsisi Tarafa ya Inyonha Wilaya ya Mlele.

Amesema kuwa miongoni mwa watu waliojeruhiwa kati yao ni watoto saba na watu wazima 11.

Aidha majeruhi wote baada ya kupelekwa katika kituo cha afya Inyonga na kupatiwa matibabu waliruhusiwa kurudi nyumbani na hali zao zinaendelea vizuri.

Kuzaga amesema kuwa chanzo cha maafa hayo ni mvua kubwa iliyonyesha ikiwa imeambatana na upepo mkali iliyosababisha kuloa kwa kuta za kanisa kisha kupelekea kuaguka.

Kwenye ajali hiyo watu waliojeruhiwa ni Meghadi Mahona(13), Adrew Masanja (7), Michael Izengo (9), Edina Maikob (13), Samwel Edward na Daniel Charles (6).

Kamanda Kuzanga amewataja majeruhi wengine kuwa ni Daudi Mahona(27), Staslaus Faustine (13), Moses Daudi (21), Rahabu Michael(8), Rahel Daudi(8) ,Paschal Michael (25),Paschal Moses (30),Eric Petro (32),Magdalena Maweja (48),Yohana Lubiza (42) pamoja na Suzana Katani (66) ambao wote ni waumini wa Kanisa hilo na wakazi wa kijiji cha Kamsisi.

Aidha Jeshi la Polisi mkoani Katavi limewaasa wananchi kuwa makini katika kipindi hiki cha msimu wa mvua kwa kuchukua tahadhari kwenye makazi wanayoishi ikiwa pamoja na kuimarisha makazi yao.