Na Esther Macha, TimesMajira Online, Mbeya
WATU 13 wamefariki Dunia na wengine 18 kujeruhiwa Mkoani Mbeya baada ya Lori aina ya scania lenye tela namba T 758 BEU scania lililokuwa limebeba kokoto kufeli breki na kugonga magari mengine ikiwemo gari la abiria aina ya Coster yenye namba T 167 DLF lililokuwa limebeba abiria kutokea Tunduma kuja Mbeya .
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 5,2024 Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa 1.30 mchana katika eneo la Mbembela katika mteremko wa Mlima Simike .
Kuzaga amesema kuwa Lori hilo lilikosa mwelekeo na kwenda kugonga gari dogo na kusababisha uharibifu kisha kwenda kugonga Coster yenye namba T 167,DLF iliyokuwa ikitokea Tunduma kwenda Mbeya ambayo ilikuwa na abiria ambako kumetokea vifo na majeruhi.
“Katika ajali hiyo kuna vifo 13 na majeruhi 18 na tunaendelea kufuatilia hali za majeruhi na dereva wa Lori amepatikana na tunaendelea kufuatilia dereva wa Guta ,bajaji pamoja na pikipiki ili kujua hali zao.
Kamanda Kuzaga amemtaja dereva wa Lori kuwa ni Ross Mwaikambo [40] na kusema Lori hilo lilitokea Shamwengo likiwa limepakia kokoto, aligongana na Gari namba T.167 DLF Toyota Coaster iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika kisha kugongana na Gari namba T.120 DER Toyota Harrier iliyokuwa ikiendeshwa na Dokta.Robert Francis Mtungi [48] Mkazi wa Isyesye.
Aidha Kamanda Kuzaga amesema Lori hilo liliendelea kugonga Guta namba MC 660 BCR iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika kisha kugonga Pikipiki namba MC 889 CKX iliyokuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika na kusababisha vifo vya watu kumi na tatu (13) kati yao wanawake 5, wanaume 8 na majeruhi [18] kati yao wanawake 4 na wanaume 14 na uharibifu wa vyombo vya moto.
Aidha Kuzaga amesema majeruhi wamepelekwa Hospitali Rufaa kanda ya Mbeya kwa matibabu na miIli ya marehemu imepelekwa Hospitalini hapo kwa hifadhi na kusubiri kutambuliwa. Chanzo cha ajali ni uzembe wa Dereva wa Gari namba T979CVV/T758 BEU kushindwa kulimudu gari kwenye mteremko.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Dereva wa Lori ambaye anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya akiwa chini ya ulinzi.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa