Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Kiwango cha watoto wenye Saratani kuishi kimeongezeka ambapo watoto wanaopona wameongezeka kutoka 35% kufikia 65% katika kipindi cha miaka 10 mfululizo kutokana na jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali na mshirika wa maendeleo Tumaini la Maisha taasisi isiyo ya kiserikali ambayo inafanya kazi kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoa huduma kwa watoto wenye Saratani.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Saratani kwa Watoto Muhimbili (Paediatric Oncology) Dkt. Rehema Laiti wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Saratani za Watoto ambayo huadhimishwa Tarehe 15 Februari kila mwaka kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu saratani za utotoni na kutoa msaada kwa watoto na vijana walio na saratani, walionusurika pamoja na familia zao.
“Saratani kwa watoto zinatibika ikiwa mtoto atawahi kufikishwa hospitali mapema, tunao watoto ambao tuliwapokea hapa wakiwa na saratani lakini baada ya kupatiwa matibabu wamepona kabisa wengine wameendelea na masomo na sasa wapo vyuo vikuu wanaendelea na masomo yao amesema Dkt. Laiti
Dkt. Laiti amesema kuwa mnamo Mwaka 2011 Wizara ya Afya, iliwahamishia rasmi watoto wanaougua saratani kutoka Hospitali ya Ocean Road kuja Hospitali ya Taifa Muhimbili. Uamuzi huu ulikua wa busara kwani matibabu ya saratani kwa watoto yanahitaji huduma nyingine mtambuka (multi-disciplinary) zaidi ya mionzi mfano uwepo wa madaktari bingwa wa watoto, madaktari wa upasuaji wa watoto, madaktari wa mifupa, madaktari wa mishipa ya fahamu, tiba kwa njia ya mazoezi, huduma za damu, maabara, huduma ya radiologia kama X–Ray, CT-Scan, MRI n.k. Pale huduma ya mionzi inapohitajika watoto hawa hupelekwa Ocean Road kupata matibabu na jioni wanarudishwa Muhimbili.
Amesema kuwa Muhimbili kwa kushirikiana na Shirika la Tumaini la Maisha wamefanikiwa Kujenga hosteli ambayo wagonjwa wanaotoka mikoani na hawana ndugu, ikiwa wanaendelea vizuri wanahitaji tu kuhudhuria kliniki hukaa hapo mpaka watakapomaliza matibabu yao, pia kuhakikisha matibabu yanatolewa kwa wakati maratu mtoto anapofikishwa Hospitalini.
“Pia tumeweza kuunda mtandao wa kutibu saratani kwa watoto ujulikanao kama (Paediatric Oncology Network) ambapo tunashirikiana kutibu watoto wenye saratani katika hospitali za KCMC, Bugando, Benjamini Mkapa, Hospitali ya Kanda Mbeya, Sengerema pamoja na Mnazi Mmoja Zanzibar,” amesema Dkt. Laiti.
Kuhusu aina za Saratani zinazoongoza kuwapata watoto nchini Dkt. Laiti amesema kuwa ni Saratani za Damu, Figo, Ngozi pamoja na Macho.
Naye Kijana Japhet Masunga (23) ambaye amenusurika na Saratani ya Figo, amesema kuwa aliaanza kuugua akiwa na umri wa miaka 10 wakati huo alikuwa akiishi na Bibi yake Wilayani Mlimba.
“Baada ya kugundulika nina saratani bibi yangu aliumia sana aliwasiliana na kaka yake ambaye alikuwa anaishi Dar es Salaam ambapo nilisafairishwa na kuletwa kuanza matibabu hatimaye sasa hivi nimepona kabisa na ninasomea masuala ya ufundi umeme,” amesema Masunga
Katika maadhimisho hayo watoto wanaougua saratani pamoja na wazazi wanaowauguza, na wale walionusurika wameshiriki matembezi ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, pamoja na michezo mbalimbali.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu