
Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online Geita
yWAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umeendelea kuonesha dhamira yake ya dhati ya kuboresha huduma kwa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa majengo ya ofisi na makazi kwa maendeleo ya Taifa.
Akizungumza mbele ya Naibu Waziri Mkuu wakati wa ziara yake katika banda la TBA kwenye Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita, Afisa Habari wa Wakala huo, Adam Mwingira, amesema TBA ipo kwenye maandalizi ya kutekeleza mradi mkubwa unaotarajiwa kuanza hivi karibuni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono maendeleo ya kitaifa.
Mwingira ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha mabadiliko ya Sheria ya Majengo kupitia Tangazo la Serikali Na. 595 la mwaka 2023, ambalo sasa linairuhusu TBA kushirikiana na sekta binafsi pamoja na taasisi za kifedha katika utekelezaji wa miradi yake.
“Kupitia sheria hii mpya, tunaweza kushirikiana kwa ubia na wawekezaji mbalimbali, jambo ambalo litaongeza kasi na ubora katika utekelezaji wa miradi yetu,tunawakaribisha wawekezaji wanaotamani kufanya kazi na TBA kushiriki nasi katika miradi hii mikubwa ya maendeleo,” amesema Mwingira.
Aidha, Afisa huyo wa Habari ametaja baadhi ya miradi muhimu inayotekelezwa na Wakala huo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, na Hospitali ya Mkoa wa Geita, ambazo amesema zimekuwa chachu kubwa katika kusogeza huduma bora za afya karibu na wananchi wa maeneo husika.
Mbali na sekta ya afya, TBA pia imefanikiwa kukamilisha miradi ya ujenzi wa ofisi mbalimbali za serikali, zikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, ambayo kwa sasa inatumika rasmi, pamoja na miradi inayoendelea kama vile ujenzi wa ofisi ya TANESCO na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi