March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa umwagiliaji Makwale kuinua kilimo, kuzima hofu ya njaa Mbeya

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mbeya

WAKULIMA wa Makwale wilayani Kyela wanatarajia kupata neema ya kilimo cha uhakika baada ya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji wa Makwale kufikia zaidi ya nusu ya utekelezaji wake.

Mradi huo unaotekelezwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa gharama ya shilingi bilioni 20.9 unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wakulima 20,000 na kufungua hekta 3,000 za mashamba, hali itakayoongeza uzalishaji wa mazao mara mbili kwa mwaka bila kutegemea mvua.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Miundombinu wa NIRC, Mhandisi Leopard Runji, alisema ameridhishwa na kasi ya ujenzi na akamtaka mkandarasi kuongeza nguvu ili mradi ukamilike kwa muda uliopangwa.

“Huu ni mradi wa kimkakati. Tunataka ukamilike kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika mapema. Ni jukumu la kila mmoja kulinda miundombinu hii, maana ni uwekezaji mkubwa kwa Taifa,” alisema Runji alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi.

Mradi huo unajumuisha ujenzi wa banio, bomba la usafirishaji maji lenye urefu wa kilomita 6.3 na mifereji mikuu na ya upili yenye zaidi ya kilomita 11.

Kwa upande wake, Mhandisi Macarius Mlayi kutoka kampuni ya Blue Mark, mkandarasi wa mradi, alisema ujenzi umefikia zaidi ya asilimia 60 na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu licha ya changamoto za mvua nyingi katika eneo la bonde.

“Changamoto zipo, lakini tumejipanga. Kwa kasi tuliyonayo na vifaa vilivyopo, tutakamilisha mradi huu kwa muda,” alisema Mlayi.

Wananchi nao wana matumaini makubwa. Bruno Benedicto Mwakalyobi, Makamu Mwenyekiti wa skimu ya Makwale, alisema mradi huo utabadilisha maisha ya wakulima.

“Tutazalisha kwa uhakika bila hofu ya mvua. Mavuno yataongezeka na maisha ya wakulima yatabadilika,” alisema.

Mradi wa Makwale ukikamilika unatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza kipato cha wakulima na kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Mbeya na taifa kwa ujumla.