March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tume ya Taifa ya Umwagiliajiyapata mafanikio ya kuhistoria

Na Imma Mbuguni, TimesMajira Online, aliyekuwa Iringa

SEKTA ya  umwagiliaji nchini imeshuhudia mafanikio makubwa ya kihistoria tangu kuanzishwa kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji mwaka 2015.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya mafanikio ya sekta hiyo iliyotolewa kwa wanahabari wa vyombo vya habari nchini.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo  jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, alisema kwa kipindi cha miaka kumi, tume hiyo imefanikiwa kuongeza eneo linalomwagiliwa kutoka hekta 461,000 mwaka 2015 hadi hekta 983,466.06 mwaka 2025, hatua ambayo imepelekea ongezeko la uzalishaji wa mazao kama mpunga, mahindi, vitunguu na nyanya yakifikia kati ya tani 5 hadi 26 kwa hekta kutoka wastani wa chini wa tani 1.5 tu.

Aidha, Mndolwa alishukuru ongezeko la bajeti katika kipindi cha miaka mitatu pekee, ambapo imepanda kutoka sh bilioni 51.49 mwaka 2021/2022 hadi sh. bilioni 403.78 mwaka 2024/2025, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 684.19.

‘Fedha hizi zimetumika kufanikisha ujenzi wa miundombinu mipya ya umwagiliaji, uchimbaji wa visima, ujenzi wa mabwawa na kutoa mafunzo kwa wakulima,” Alisema Mndolwa.

Tume imefanikiwa kuajiri watumishi 340, kununua magari 58, mitambo 30 na mashine 17 za kuchimba visima, pamoja na kuanzisha ofisi za wilaya 121 kote nchini ili kuongeza usimamizi wa karibu.

Jumla ya miradi 780 ya umwagiliaji inaendelea kutekelezwa mwaka huu wa fedha 2024/25, ambayo ni pamoja na miradi mipya 63 ya ujenzi, ukarabati wa skimu 48, na ujenzi wa mabwawa 14, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha wakulima wanapata maji ya uhakika kwa ajili ya uzalishaji wa chakula na malighafi.

Aidha, idadi ya vyama vya umwagiliaji vimesajiliwa kuongezeka kutoka 175 mwaka 2019 hadi 909 mwaka 2025, jambo linalodhihirisha mwitikio mkubwa wa jamii kwenye kilimo cha kisasa.

Katika mipango ya muda mrefu, Serikali inalenga kuongeza eneo linalomwagiliwa hadi kufikia hekta milioni 5 ifikapo mwaka 2030, huku sekta hiyo ikitarajiwa kuchangia asilimia 50 ya mahitaji yote ya chakula nchini, na kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa.

Kwa sasa, Tanzania ina hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini ni asilimia 2.5 tu ya eneo hilo ndilo linalotumika. Hii inatoa fursa kubwa ya maendeleo endapo uwekezaji utaendelea kuongezwa katika sekta hiyo.

Sekta ya umwagiliaji inaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuhakikisha usalama wa chakula, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake, na kukuza upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya ndani.

Tume imeahidi kuendeleza juhudi za ujenzi wa mabwawa mapya, uchimbaji wa visima, na matumizi ya teknolojia bora kuhakikisha tija inaendelea kupanda.