April 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yazindua huduma matibabu ya macho bure mkoani Mbeya

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya mawasiliano nchini, YAS kwa kushirikiana na KSI Charitable Eye Centre, imezindua rasmi kampeni ya siku tatu ya huduma ya matibabu ya macho bure kwa wakazi wa Jiji la Mbeya na maeneo ya jirani.

Mpango huo, ulianza kutekelezwa Aprili 18 hadi 21, mwaka huu, unalenga kusaidia jamii zisizopata huduma za afya ya macho kwa urahisi kutokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson (katikati mwenye miwani), ni miongoni mwa walihudhuria katika uzindua rasmi wa kampeni ya siku tatu ya huduma matibabu ya macho bure kwa wakazi wa Jiji la Mbeya na maeneo ya jirani.

Uzinduzi wa kampeni hiyo ulifanyika katika hafla maalum iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali, wadau wa sekta ya afya, wawakilishi wa sekta binafsi, wananchi pamoja na wageni waalikwa.

Akizungumzia huduma hiyo Meneja wa Masoko ya Biashara wa YAS, Eric Charles amesema ushirikiano wao na KSI Charitable Eye Centre, wametoa huduma hizo bure kwa siku tatu mfululizo kwa wote wanaohitaji matibabu ya macho.

“Tunaamini kwa dhati kuwa afya bora ya macho ni kichocheo cha maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Kampeni hii itanufaisha watu wanaosumbuliwa na matatizo kama mtoto wa jicho.

“Lakini pia, pamoja na wale wanaofanya kazi hatarishi kama wachomeleaji vyuma na waendesha bodaboda ambao mara nyingi hupuuza matumizi ya vifaa kinga,” amesema Eric Charles.

Aidha, amesema huduma zinazotolewa ni pamoja na uchunguzi wa kina wa macho, matibabu ya magonjwa mbalimbali ya macho, ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa wa macho, pamoja na upasuaji kwa wagonjwa watakaohitaji huduma hiyo.

Pia, amesema washiriki walipata elimu kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya maradhi ya macho kwa kutumia vifaa kinga na kuhakikisha mazingira salama kazini.

Hata hivyo amesema, zoezi hilo la Mbeya ni sehemu ya kampeni ya kitaifa inayoendelea inayotekelezwa na YAS na KSI Charitable Eye Centre kwa lengo la kufikisha huduma za macho kwa jamii mbalimbali nchini, baada ya mafanikio katika maeneo ya Zanzibar, Mtwara, Tanga na Mkuranga.

“YAS itaendelea kuwa karibu na jamii kuhakikisha upatikanaji jumuishi wa huduma bora za kijamii na mawasiliano. Huduma hizi za afya si msaada wa muda tu — ni sehemu ya dhamira yetu ya kizalendo ya kuboresha maisha ya Watanzania,” amesema Charles.

Wakazi wa Mbeya na maeneo ya jirani walihamasishwa kujitokeza kwa wingi katika vituo vilivyotengwa ili kunufaika na huduma hizi za bure za macho, na kuwahamasisha ndugu na marafiki kushiriki pia.