Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
USAJILI wa walimu wa daraja la 3C Kiswahili uliopangwa kufanyika leo Januari 28, mwaka huu nchi nzima umeahirishwa hadi Januari 30.
Usaili wa walimu unawahusisha walimu 201,707 walioomba ajira serikalini wakipigania nafasi 14, 2025 zilizotangazwa na Serikali na unatarajiwa kumalizika Februari 24, 2025.
Kuahirishwa kwa usaili wa walimu hao unatokana na Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu nishati. Mkutano huo ulioanza jana unatarajiwa kumalizika leo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na Katibu wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Lynn Chawala, mabadiliko hayo yametokana na kufungwa kwa baadhi ya barabara jijini Dar es Salaam kwa muda.
Alisema hali hiyo inaweza kusababisha changamoto kwa wasailiwa kufika katika vituo vyao vya usaili kwa wakati.
“Usaili wa walimu wa daraja la 3C Kiswahili uliopangwa kufanyika Januari 28, 2025, katika vituo mbalimbali nchini sasa utafanyika Januari 30, kuanzia saa 1:00 asubuhi.
”Mabadiliko hayo yametokana na uwepo wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati, utakaofanyika jijini Dar es Salaam, uliosababisha kufungwa kwa baadhi ya barabara Januari 27 na 28, 2025,” ilieleza taarifa hiyo.
Alisema mabadiliko hayo yanalenga kuepusha changamoto ya usafiri kwa wasailiwa wanaotoka Dar es Salaam, ili kuhakikisha wanawahi kufika vituoni kwa wakati.
Hata hivyo, tarehe nyingine za usaili, mahali pa kufanyia usaili, na muda wa usaili, vimebaki kama ilivyoainishwa kwenye matangazo ya awali ya kuitwa kwenye usaili.
More Stories
Tuzo za EAGMA zazinduliwa rasmi
Katibu Mkuu Nishati aipongeza Sweden kufadhili miradi ya umeme nchini
RAS Seneda akabidhi msaada wa Mablanketi kwa wazee na yatima