December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zahanati ya Kiiiii cha Nyabaengere yaanza kutoa huduma

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Mara.

WANANCHI wa Kijiji cha Nyabaengere Kata ya Musanja Wilaya ya Musoma Mkoani Mara,   wameanza kunufaika na Huduma za Afya ambazo zimeanza kutolewa katika Zahanati ya Kijiji chao na hivyo  kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kwenda kupata Huduma hizo kwenye Kata Jirani ya Murangi.

Ujenzi wa Zahanati hiyo umehusisha  Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Sospter Muhongo, michango ya fedha za Wananchi na nguvu kazi zao, Viongozi wa kata, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma na fedha kutoka serikali kuu. 

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Disemba 6,  2024,imeyabainisha hayo na kuongeza kuwa,  Utoaji wa Huduma za Afya umeendelea  kuboreshwa ndani ya vijiji vya Jimbo hilo na kuwapa uhakika wa Huduma za Afya Wananchi.  

“Kata ya Musanja yenye vijiji vitatu (Mabuimerafuru, Musanja na
na Nyabaengere. Vijiji viwili  (Nyabaengere na Mabuimerafuru) vinajenga zahanati za vijiji vyao. Na leo  Kijiji cha Nyabaengere kimezindua utoaji wa Huduma za Afya kwenye zahanati yake mpya.”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Ujenzi  wa Zahanati  hiyo ulianza kupitia Harambee ya Mbunge wa Jimbo Prof. Sospter Muhongo kuchangia mifuko  100  ya Saruji,  pia  kwa kukusanya michango na nguvu kazi za wanakijiji na viongozi wao. 

Pia, Diwani na Wanakijiji walichangia  michango yao yenye  takribani Shilingi Mil. 5,  Wazaliwa wa Kijiji cha Nyabaengere nao  wamechangia jumla ya Shilingi 400,000.

“Baadae, Halmashauri yetu (Musoma  DC ) ilichangia Shilingi Mil. 50. Na
vilevile, Serikali Kuu ilichangia Mil. 50, huduma za afya zimeanza kutolewa.  Huku  ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu inayohitajika unaendelea.”imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Wananchi wa Kijiji  hicho na Jimbo la Musoma Vijijini kwa ujumla, wameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuchangia fedha nyingi za  utekelezaji wa miradi ya Maendeleo katika Vijiji mbalimbali jimboni humo. 

“Nafurahi kuona Huduma za Afya zinatolewa kwenye Zahanati hii ambapo  tutakuwa tunapata matibabu ya kawaida  hapa hapa badala ya kutembea kwenda Murangi. Haya yote ni mageuzi makubwa sana ambayo tumeendele kuyapata jimboni mwetu  yakichangiwa na uhodari wa Mbunge wetu Prof. Muhongo,  pia  Rais wetu Dakt.  Samia Hassan ambaye amekuwa akitoa fedha za  ujenzi wa miradi ya maendeleo.”amesema Mafuru Juma Mkazi wa Nyabaengere.