Na Lubango Mleka,TimesMajiraOnline,Igunga
WAZAZI waliojifungua watoto kabla ya wakati wameshauriwa kuwa na subira wanapokuwa Hospitalini kwa ajili ya kupatiwa huduma.
Ushauri huo umetolewa na Rehema Iddi mkazi wa Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora leo Novemba 20,2024 katika hafla fupi iliyohusisha Madaktari, Wauguzi na Wazazi waliojifungua watoto kabla ya wakati,
“Napenda kuwashauri Wazazi wenzangu tunapokuwa wodini tusiwe na haraka ya kurudi nyumbani, haraka inaweza kusababisha athari kubwa kwa mtoto hata kifo” amesema Rehema.
Ameendele kusema kuwa, alijifungua watoto mapacha mmoja alikuwa na uzito wa 1kg na mwingine 1.1kg na amekaa wodini kwa siku 48 akisaidiana na wauguzi na Madaktari katika kuwahudumia.
“Mtoto mmoja Mungu alimchukua na niliye naye hadi natoka Hospitalini alikuwa na uzito wa 2Kg, naishukuru Hospitali ya Rufaa ya Nkinga kwa huduma nzuri aliyonipatia kupitia Wauguzi na Manesi, sasa hivi mtoto wangu ana umri wa miezi 10 na uzito wa 7kg,”amesema Rehema.
Ameongeza kuwa, “Watoto hawa wanahitaji uangalifu sana, hawahitaji baridi na wala hawahitaji joto kali, mzazi ukiwa nyumbani inakuwa ngumu kutambua haya.”
Aidha, Rehema amewashauri Wazazi kuendelea kuwapa ushirikiano Wauguzi na Madaktari wanapokuwa Hospitalini kwa kusikiliza ushauri wao.
Mkuu wa idara ya watoto (Paediatric) katika Hospitali ya Rufaa ya Nkinga na Daktari bingwa wa watoto Jacqueline Suba amesema, licha ya watoto hao kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika ukuaji wao,
Pia wanakabiliwa na changamoto ya kujisahau kupumua katika kipindi cha sekunde 20 hivyo mama akiwa nyumbani ni vigumu kumuhudumia kwakuwa atahitaji kukaa kwenye Oxygen.
Hafla hiyo imejiri katika kuadhimisha siku ya mtoto aliyezaliwa kabla ya wakati inayofanyika Novemba 17 kila mwaka, ambapo Hospitali ya Rufaa ya Nkinga kupitia idara ya watoto (Paediatric) imeona vema kuiadhimisha kwa kukumbushana mambo kadhaa na watendakazi wa idara zingine na wazazi waliojifungua watoto hao.
More Stories
Issa Gavu atua Geita kuzindua kampeni leo
Rais Samia ayapa ushauri Mataifa ya G20
Rais Samia aongeza saa 24 uokoaji Kariakoo