September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Yonazi akutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa PSARP

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt.Jim Yonazi amekutana na kufanya mazungumzo na Mratibu wa Mpango wa Ulinzi wa Usalama na Utatuzi wa Mashambulizi (Protective Security & Attack Response Programme – PSARP) chini ya Ubalozi wa Uingereza kuhusu uwezekano wa kuandaa Mpango wa Kuimarisha Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Maafa.

Amekutana nao mwishoni mwa wiki walipomtembelea Ofisi kwake Jijini Dodoma na kueleza kuwa PSARP inalengo la kuimarisha uwezo wa Wataalam katika kukabiliana na maafa nchini.     
                     
Katika mazungumzo hayo, Dkt.Yonazi ameshukuru uongozi huo kwa kumtembelea na kutumia fursa hiyo kujadili majukumu ya msingi ya Ofisi yake ya kuratibu Shughuli za Serikali ikiwa ni pamoja na uratibu wa masuala ya maafa nchini ambalo ndilo eneo walilolenga kuzungumza na kuona namna bora ya kushirikiana na Serikali.

Kwa upande wake Mratibu wa Mpango wa Ulinzi wa Usalama na Utatuzi wa Mashambulizi (PSARP) – Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara John Spencer ameipongeza Serikali kwa namna inavyoendelea kutekeleza majukumu yake ikiwemo suala la menejimenti ya maafa huku akielea lengo la Mpango wa Ulinzi wa Usalama na Utatuzi wa Mashambulizi ambao umejikita katika kuimarisha utendaji wa polisi katika operesheni za dharura na kuona fursa katika kushirikiana na nchi ya Tanzania ili kuimarisha utendaji wa pamoja wa taasisi zinazohusika na kukabiliana na maafa.

Aliongezea kuwa wapo tayari kushirikiana ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha uwezo wa kukabiliana na maafa kwa kuwajengea uwezo wataalam wa maafa katika eneo la mfumo jumuishi wa utendaji wa pamoja wakati wa dharura