September 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kapinga: Damira ya Rais Samia ni kuona wananchi wananufaika na miradi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Mtwara

NAIBU Waziri Nishati, Judith Kapinga, amesema kuwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao.

Kapinga alisema hayo juzi wilayani Mtwara Mkoa wa Mtwara wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyolenga kukagua visima vya kuzalisha gesi asilia katika eneo la Mnazi Bay pamoja na miradi inayofanyika kwa manufaa ya jamii kutokana na uwepo wa gesi hiyo (CSR) ikiwemo ujenzi wa kituo cha Afya na kituo cha Polisi katika eneo la Msimbati.

“Yote haya mnayoyaona ni matunda ya kazi nzuri ya Rais Samia ambaye anaonesha kwa vitendo jinsi anavyowajali kwa kuhakikikisha mnapata huduma bora kupitia miradi hii.” Alisisitiza Kapinga.

Alieleza kuwa lengo la ziara hiyo ya Kamati ya Bunge ni kujionea thamani ya miradi hiyo ambayo itanufaisha wananchi wa Msimbati, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko aliyoyatoa Novemba 15, 2024 mara baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na wananchi.

Alisema ujenzi wa kituo cha afya unatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2024 huku ujenzi wa Kituo cha Polisi nao ukiwa ukingoni.

Kapinga alisisitiza kuwa, Serikali ipo pamoja na wananchi katika kuhakikisha inawapelekea maendeleo.

Katika hatua nyingine, Kapinga aliwaasa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa kwa kuanza kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.