*Ni pamoja na mwenyeji wake Rais wa Korea, pia washuhudia kusainiwa hati mbili za makubaliano, tamko la kuanzishwa EPA
Na Mwandishi Wetu, TimemajiraOnline, Korea
RAIS Samia suluhu Hassan na Rais Yoon Suk Yeol wa Jamhuri ya Korea wameshuhudia utiaji saini wa mkataba mmoja, Hati za
Makubaliano (MOU) mbili na Tamko la Pamoja la kuanzisha Mkataba wa Ushirikiano wa Uchumi (EPA).
Mkataba huu utaiwezesha Tanzania kupokea mkopo kutoka Korea wa kiasi cha Dola za Kimarekani Bilioni 2.5 kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia (2024- 2028).
Fedha hizo kwa ajili ya miradi ya miundombinu ya maendeleo zinatolewa chini ya Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Serikali ya Korea (EDCF).
Ili kufungua milango zaidi ya ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi, Tanzania na Korea zimesaini pia mkataba wa EPA utakaowezesha kuufanya uhusiano kuwa wa kimkakati hususan katika Nyanja za Biashara, Uwekezaji, Viwanda, Usafirishaji nakadhalika.
Tanzania ni miongoni mwa nchi tatu tu barani Afrika ambazo zitafanya majadiliano hayo yatakayozaa Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Korea.
Nchi zingine ni Morocco na Kenya. Hati za Makubaliano zilizotiwa saini jana ni pamoja na Ushirikiano katika Uchumi wa Buluu, ambapo Tanzania itashirikiana na Korea Kusini katika maeneo ya uvuvi, viwanda vya kuchakata mazao ya bahari, ujenzi wa bandari za uvuvi, teknolojia na tafiti za masuala ya
bahari.
Vile vile, Wizara ya Madini ya Tanzania na Wizara ya Biashara, Viwanda na Nishati ya Korea Kusini zimetia saini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano katika Madini ya Kimkakati.
Tanzania na Korea Kusini zitashirikiana katika utafiti, uwekezaji, uchimbaji na kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya madini ya kimkakati nchini Tanzania. Madini hayo ni Nickel,
Lithium na Kinywe.
Wakati huo huo, Rais Samia amependekeza ushirikiano wa sekta nyingine mpya zikiwemo maendeleo ya nishati ya gesi asilia; sekta ya Ubunifu ikiwemo sanaa na filamu; na kufunguliwa kwa soko la ajira la nchini Korea kwa vijana wa Tanzania kupitia mpango wa Employment Permit System (EPS).
Rais Samia amehitimisha ziara rasmi ya siku mbili 2, na anatarajia kuanza ziara ya kikazi ambapo atahudhuria mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kati ya Korea na Afrika.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa