November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania, Standard Chartered yateta ujenzi SGR

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online

BENKI ya Standard Chartered ipo katika hatua za mwisho za utaratibu wa kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa vipande vilivyobakia vya reli ya kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR) ikiwa ni pamoja na kipande cha Makotopora-Tabora, Tabora – Isaka, Isaka-Mwanza na kipande cha kuanzia Tabora hadi Kigoma.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Standard Chartered anayesimamia nchi za Afrika na Mashariki ya Kati, Sunil Kaushal.

Dkt. Nchemba amesema kuwa Tanzania na Benki ya Standard Chartered, imekuwa na ushirikiano mzuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya reli ambayo inaendelea vizuri.

“Tumekuwa na majadiliano kuhusu vipande vya reli ambavyo taratibu za kupata fedha zilikuwa hazijakamilika kikiwemo kipande cha Makotopora-Tabora, Tabora – Isaka, Isaka-Mwanza na kipande cha kuanzia Tabora hadi Kigoma”, amesema Dkt. Nchemba

Dkt. Nchemba amemshukuru Mkurugenzi huyo na timu yake kwa ujumbe waliouleta ambao unaeleza kuwa Benki hiyo ipo kwenye hatua za mwisho za taratibu za kupata fedha kwa ajili ya vipande hivyo vya Reli

Amesema kuwa Reli ni miongoni mwa miradi ya kipaumbele katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na mara zote amekuwa akiuliza upatikanaji wa fedha umefikia hatua gani

Alisema kuwa kwa sasa anayofuraha kumpelekea ujumbe, Mhe. Rais kuwa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vipande hivyo umefikia hatua nzuri.

Dkt. Nchemba ameziagiza timu za wataalam zinazoshughulikia jambo hilo kuhakikisha zinafanya taratibu za ukamilishaji wa upatikanaji wa fedha hizo ili miradi iende kwa kasi ambayo watanzania wanaitarajia.

Aidha ameipongeza timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango kwa kukamilisha masuala mbalimbali yaliyokuwa yamejitokeza likiwemo suala la mazingira ambalo limepatiwa ufumbuzi

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benkia nchi za Afrika na Mahariki ya Kati, Sunil Kaushal, amesema kuwa Tanzania inafanya juhudi kubwa katika kusimamia uchumi na pia inafursa nyingi za uwekezaji ikilinganishwa na nchi nyingi za Afrika.